TIMU ya Azam FC kesho saa 10 jioni itashuka kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, hapa Mtwara kuvaana na Ndanda, huku wakiwa wamepania kuibuka na ushindi na kulipa kisasi cha kufungwa msimu uliopita mkoani hapa.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ilikutana kwa mara ya kwanza na Ndanda msimu uliopita na kupoteza kwa bao 1-0 lakini Wanalambamba hao walipata ushindi kama huo ziliporudiana Uwanja wa Azam Complex, bao lililofungwa na Gaudence Mwaikimba aliyehamia JKT Ruvu msimu huu. 

Mchezo huo unatarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na matokeo ya nyuma ya timu hizo, Azam FC ikiwa haijafungwa mechi yoyote kati ya sita ilizocheza mpaka sasa huku Ndanda ikiwa haijafungwa katika uwanja wake wa nyumbani kwenye mechi mbili walizocheza, moja ikiifunga Coastal bao 1-0 na kulazimishwa suluhu na Toto Africans ya Mwanza.

Lakini Azam FC ina rekodi nzuri msimu huu kwenye mechi za ugenini msimu huu ikishinda zote mbili ilizocheza mkoani Shinyanga kwa kuzichapa Stand United mabao 2-0 na Mwadui 1-0. 

Katika mechi nyingine zilizobakia Azam FC imezifunga Tanzania Prisons (2-1), Mbeya City (2-1), Coastal Union (2-0) kabla ya kutoa sare ya 1-1 dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.

Akizungumzia mechi hiyo Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema utakuwa mgumu kutokana na Uwanja wa Nangwanda kuwa mbovu huku akidai kuwa itamlazimu atumie mipira mirefu ili kuweza kukabiliana na hali mbaya ya uwanja huo.

“Natarajia mchezo mgumu kwani wapinzani wetu hawajapoteza mchezo wa nyumbani mpaka sasa, na wao wanajua kuwa lazima washinde mechi za nyumbani ili kuweza kubakia kwenye ligi, ila tumejipanga kushinda,” alisema.

Mwingereza huyo alisema katika mchezo huo atawakosa nyota wake kama winga Farid Maliki, viungo Mudathir Yahya na Kipre Balou, ambao ni wagonjwa huku kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akikosekana kutokana na kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kukusanya kadi tatu za njano mfululizo.

“Pia nitampumzisha kipa Aishi Manula kutokana na kutokuwa fiti, nitamwanzisha Mwadini (Ali)… Naweza nikamchezesha Aishi lakini tunakabiliwa na mechi tatu ngumu ndani ya siku 10, hivyo sitaki apate majeraha yatakayomfanya tumkose kwa muda mrefu zaidi,” alisema.

Hall aliyeipa ubingwa wa Kombe la Kagame timu hiyo Agosti mwaka huu, ameongeza kuwa kukosekana kwa nyota hao hakumpi shida kutokana na ubora wa kikosi chake alichokuwa nacho, amedai kuwa kwenye sehemu ya kiungo anaweza kumtumia Ramadhan Singano ‘Messi’ ili kuziba pengo la Sure Boy kama alivyomchezesha katika mchezo uliopita dhidi ya Yanga kipindi cha pili.

Azam FC yenye pointi 16 inahitaji ushindi tu ili kuifikia Yanga iliyofikisha pointi 19 leo baada ya kuifunga Toto Africans mabao 4-1.  

Pia itakuwa ni fursa nyingine kwa mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche, mwenye mabao manne mpaka sasa kwenye ligi, kuendeleza moto wake wa kufunga mabao baada ya kufunga katika mechi tatu mfululizo zilizopita.

Ndanda FC nayo inaye mshambuliaji Atupele Green, anayeongoza kuifungia mabao timu hiyo akiwa amefunga mawili mpaka sasa.