Uamuzi mbovu wa kubabaika na usiozingatia sharia 17 za soka wa mwamuzi Abdallah Kabuzi umeharibu pambano la ligi kuu Tanzania kati ya Azam FC na Yanga SC zilizotoka sare ya kufungana bao 1-1

 

Mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Matokeo hayo yanazifanya Yanga SC na Azam FC ziendelee kuongoza ligi kwa wastani wa mabao, zikiwa na pointi 16 kila moja.

 

Hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa Zimbabawe, Donald Ngoma dakika ya 45 za kipindi cha kwanza.

Ngoma alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi ya Malimi Busungu, ambaye naye alipokea mpira mrefu wa beki wa kulia, Juma Abdul, Yanga SC ikitoka kushambuliwa.

Mshambuliaji Mkenya wa Azam FC Allan Wanga, alijaribu kuunganisha kwa kichwa cha mkizi krosi ya John Bocco, lakini mpira ukaenda nje dakika ya 19 na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliingia vizuri kwenye eneo kla hatari la Yanga SC, lakini Mwinyi Hajji Mngwali akatokea na kuokoa.

 
Kipindi cha pili, Azam FC ambayo kipindi cha kwanza ilipwaya ilibadilika na kuanza kucheza kwa kujiamini baada ya mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche kuingia kuchukua nafasi ya Allan Wanga, Ramadhan Singano kuingia kuchukua nafasi ya Salum Abubakar na Kipre Bolou kumpisha Frank Domayo Chumvi.

Na ni Kipre Tchetche huyo huyo aliyekwenda kuisawazishia bao Azam FC dakika ya 82 akimchambua vizuri Ally Mustafa ‘Barthez’ baada ya kupokea pasi ya Farid Mussa.

 

Katika hali ya kustaajabisha, mwamuzi wa mchezo wa leo aliwazawadia Yanga penati ya maajabu, kwani Simon Msuva alimtoka beki, David Mwantika akamchambua kipa Aishi Manula lakini mpira wake ukakutana na beki aliyefika golini na kuuokoa lakini kwa mastaajabu ya wengi, Refa Kambuzi akaamuru mkwaju wa penalti, ambao wachezaji wa Azam FC walipingana naye kwa dakika zaidi ya moja, kabla ya kukubali kwa shingo upande na Aishi akainusuru timu yake kuzama. 
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Cannavaro, Mbuyu Twite/Said Juma ‘Makapu’ dk78, Salum Telela/Deus Kaseke dk89, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Malimi Busungu/Simon Msuva dk56. 

Azam FC; Aishi Manula, Aggrey Morris, David Mwantika, Serge Wawa Pascal, Shomary Kapombe, Farid Mussa Shah Malik, Kipre Balou/Frank Domayo dk69, Himidi Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk57, Allan Wanga/Kipre Tchetche dk63 na John Bocco.