Azam FC na Yanga SC zimejenga upinzani mkubwa uwanjani kiasi cha kufanya mechi kati ya timu hizi inapokaribia kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka nchini.

 

Wapo wanaoamini kuwa, ukitaka kushuhudia soka la kiwango cha juu toka kwa timu zenye wachezaji wenye viwango vizuri zaidi nchini tazama mechi kati ya Azam FC na Yanga.

 

Hisia hizi zinapata nguvu kutokana na mafanikio ya vilabu hivi kwenye miaka ya karibuni. Yanga ndiye bingwa mtetezi wa Tanzania huku Azam FC akiwa makamu bingwa na bingwa wa CECAFA Kagame Cup.

 

Lakini kama vile rekodi hizo hazitoshi, rekodi za usajili pia zinaonesha kuwa wachezaji nyota nchini wamekuwa wakiangukia kwenye mikono ya Azam FC na Yanga. Huku viongozi wa klabu hizi wakiwa makini sana kwenye kuajiri wachezaji wa kigeni na wakufunzi.

 

Msimamo wa ligi kuu msimu huu unaonesha kuwa Azam FC na Yanga SC ndizo klabu ambazo hazijapoteza mchezo hata mmoja tangu ligi ianze zikicheza michezo saba na kushinda yote saba.

 

Kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Azam FC na Yanga zina wachezaji wengi zaidi ambapo kwenye mechi iliyopita kila timu ilianzisha wachezaji wane. Wachezaji toka Yanga walikuwa ni Ally Mustapha Bartez, Hajji Mwinyi Mgwai, Nadir Harou na Kevin Patrick Yondani huku Azam FC ikichangia Shomari Kapombe, Himid Mao, Mudathir Yahya na Farid Mussa Shah.

 

Mechi itakazozikutanisha Azam FC na Yanga itakuwa mechi ya kuamua ubishi uliopo wa nani anastahili kujitawala kileleni.

 

Nani atapoteza mechezo huo? Hilo ni swali ambalo mashabiki wengi wa soka nchini wanasubiri majibu toka uwanjani jumamosi hii.