Wagonga nyundo wa jiji la Mbeya MCCA wana poiti tatu tuu baada ya kupoteza michezo miwili na kushinda mmoja. Mchezo wa tatu kwao wanakuja Chamazi Complex wakiwa na malengo ya kurejesha imani kwa mashabiki wao wakorofi na kuweka matumaini hai ya kutwaa ubingwa kama walivyojinasibu.

 

Tambo za Mbeya City ni kuwa bada ya misimu miwili ya uzoefu, sasa ni wakati wao lakini msimu walioutegemea kama msimu wao wameanza vibaya na wanahitaji kurekebisha hali hii haraka sana.

 

Kwa mabingwa wa Kagame Cup Azam FC, ushindi wa 100% ni muhimu sana kwani vinara wa ligi kuu Yanga SC na Mtibwa Sugar FC wameshinda mechi nne mfululizo na Azam FC isingependa kuwaacha Yanga na Mtibwa wakitanua kileleni.

 

Ugumu wa ligi ya msimu huu ni kutokana na uweli kwamba nafasi yenya maana ni ya kwanza tu. Nafasi ya pili haina maana tena kwani FA CUP imerudi chini ya udhamini wa Azam TV na kuondoa nafasi ya makamo bingwa kushiriki kombe la shirikisho.

 

Mwaka huu ligi ni ngumu sana, Simba wana kikosi kizuri na wameimarika, Yanga SC wana kikosi kizuri, Mtibwa Sugar wameanza kwa makeke na wana uwezo wa kifedha na uzoefu kuleta upinzani. Mbeya City wanaamini huu ni msimu wao huku kukiwa na vilabu kama Mwadui FC, Stand United, Kagera Sugar, Coastal Union na Majimaji ambavyo vina uwezo wa kifedha na dhamira ya kufanya vizuri.

 

Azam FC ina majeruhi wawili tuu, Khamis Mcha Khamis maarufu kama Viali wa Unguja na Kipre Bolou. Lakini wachezaji wengine wote wapo kwenye hali nzuri na wamejiandaa vema na mchezo chini ya kocha mzoefu mwenye ujuzi mwingi Stewart John Hall.

 

Azam FC na Mbeya City zina kumbukumbu ya mchezo bora wa kihistoria uliomalizika kwa matokeo ya sare ya 3-3. Mwagane Yeya akifunga goli zote tatu kwa upande wa Mbeya City huku Humfrey Mieno, John Bocco na Khamis Mcha wakifunga kwa upande wa Azam FC.

 

Mechi hii ilikuwa ya kwanza kuzikutanisha Azam FC na Mbeya City lakini imebaki kuwa kwenye kumbukumbu kama mechi bora zaidi kuwahi kufanyika Chamazi Complex.

 

Je? Leo tutaona marudio ya mechi hii bora? Mwamuzi ni dakika 90