Baada ya Azam FC kuchukua ubingwa wa Kombe la Kagame bila kuruhusu goli hata moja kutinga kwenye nyavu zake.  Kocha mkuu wa kikosi hicho, Muingereza Stewart John Hall (Mourinho) amesema, safu yake ya ulinzi imekuwa imara kwa sababu  ndiko alianza nako na aliamini patampa mafanikio kwa sababu safu hiyo ni sawa na msingi wa nyumba.

 

Lakini amesisitiza kuwa bado hajapata soka analolitaka, soka la kutiririka na pasi za haraka haraka za vuvutia, hivyo basi anakwenda mafichoni kujipanga upya na atakaporudi timu itakuwa moto wa kuotea mbali.

 

Sambamba na kuboresha kikosi pia kwenye ushambuliaji anataka wachezaji wawe na makali na atakaporudi kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga wapenzi wa soka wategemee kitu kingine kipya na wanaodhani ni nguvu ya soda, wakae mkao wa kula.

 

Stewart alisema: “Timu ilikuwa imara kwenye ulinzi kwa sababu ndiko nilianza nako kutengeneza kama unavyojua, safu ya ulinzi kwenye timu naweza kuifananisha na msingi unapoanza kujenga nyumba, unapokosea kuanzia hapo kila kitu kinaharibika.”

 

“Hivyo baada ya kukamilisha hili, sasa nakwenda kujiandaa na Yanga, huko nitaboresha pia safu nyingine ambazo zina mapungufu tukirudi, kila kitu kitakuwa safi,”alisema Stewart.

 

Azam FC imechukua Kombe hilo baada ya kushiriki mara mbili kwa nyakati tofauti, lakini imeweka historia tangu ianze mashindano haijaruhusu hata  bao moja la kufungwa.

 

Safu yake ya ulinzi, iliyokuwa chini ya Waziri wa Ulinzi Serge Wawa, Aggrey Morris, Said Morrad, Gardiel Michael, Abdallah Kheri, Shomari Kapombe, Farid Mussa na Erasto Nyoni huku viongo Jean Baptiste Mugiraneza na Himid Mao wakicheza eneo la kiungo cha ulinzi. Stewart Hall anasisitiza, ulinzi huo ulifanywa na wachezaji wote 11 waliokuwa wanacheza kwenye timu.