Ratiba ya robo fainali ya mashindano ya kombe la Kagame inaonesha kuwa Azam FC itacheza na Yanga Jumatano.  Kocha Stewart Hall amesema, vijana wake wako tayari kiakili, kimwili na kimbinu, akatamba “Yanga tukutane uwanjani”.

 

Stewart amesema, anafahamu Yanga ni timu kubwa na inamashabiki wengi, hivyo mbali na kucheza na timu ya uwanjani, atakuwa na kibarua kingine dhidi ya wapenzi hao lakini haimtishi, anaijua, ameizoea na safari hii hatawapa nafasi.

 

“Kama tulivyoanza na ndivyo tutakavyopambana na Yanga. Ni kweli Yanga ni timu kubwa na ina mashabiki wengi yote ni changamoto, lakini  kwangu mimi sijali,”alisema Stewart.

 

“Kitu cha kwanza ninachoangalia ni timu yangu  ambayo kwa asilimia zote iko vizuri na ninachokifanya sasa ni masahihisho madogomadogo tu.” Ni jambo lililowazi kuwa Azam FC ni bora kuliko Yanga kwa sasa.