Straika Muivory Coast Kipre Tchetche aliyekuwa anaingia ‘sabu’, kesho ataanza kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha Azam FC kitakachoivaa Adama City ya Ethiopia katika mechi ya muendelezo wa mashindano ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Tchetche atacheza straika kuchukua nafasi ya John Bocco ‘Adebayor’ ambaye atakuwa jukwaani kama shabiki na pacha atakayecheza naye kwa mfumo wa 3-5-2 atakuwa Ame Ally au Mrundi Didier Kavumbagu.

 

Kocha mkuu wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall amesema, atampumzisha Bocco ili awe tayari kwa mechi ya robo fainali kwa sababu tayari wameshafuzu.

 

“Tchetche ataanza mechi ya kesho kwenye kikosi cha kwanza na nitamchezesha na Kavumbagu au Zungu, yoyote kati ya hao wawili atakayeamka vizuri.

 

“Nitampumzisha pia, kipa Aishi Salum na golini atasimama Mwadin Ally na kwenye kiungo, Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ naye atapumzika, yeye ana maumivu ya enka,”alisema Stewart.

 

Stewart amesema maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri na kila kitu kinakwenda sawa na msimu huu, anataka kulibakisha kombe la Kagame Chamazi.

 

Tangu michuano hiyo ianze, Tchteche alikuwa mchezaji wa akiba na alikuwa akiingia kipindi cha pili, hivyo mechi hiyo itakuwa ya kwanza kuanza kwake.