Ikicheza soka la kiwango cha juu na kuvutia Azam FC leo imeifunga Malakia ya Sudan Kusini 2-0 shukrani kwa magoli ya John Bocco dk 27 na Kipre Tchetche dk 52.

Bocco alifunga goli hilo kwa mpira wa adhabu ndogo alioupiga kwa ustadi mkubwa sana na goli la Kipre Tcheche lilitokana na kazi nzuri ya Shomari Kapombe aliyewazidi maarifa walizi wa tatu wa Malakia na kutoa pasi kwa mfungaji ambaye hakufanya ajizi kwa kuukwamisha mpira kwenye nyavu.

Azam FC ambayo inafundishwa na mwalimu mwenye uzoefu na weledi wa hali ya juu Stewart Hall, imebadili mfumo wa uchezaji toka 4-3-3 na sasa inatumia mfumo wa 3-5-2  leo imeutendea haki mfumo huo kwa kucheza kwa kuelewana na kwa ustadi mkubwa.

Ukilinganisha na muda uliotumika kuandaa timu, sifa za kipekee ziende kwa kocha Stewart Hall na benchi lake la ufundi pamoja na wachezaji wote ambao bila shaka wamefanya kazi kubwa sana.

Wachezaji wote leo wametimiza majukumu yao lakini sifa za kipekee ziende kwa mchezaji kinda na mgeni kwenye kikosi cha kwanza Abdallah Kheri SEBO ambaye  amecheza kwa kiwango kikubwa sana.

Azam FC sasa imetimiza pointi sita na inaongoza kundi lake.