Mkenya aliyekuwa akikipiga na El Marrikh ya Omduman Sudan, Allan Wanga yupo Makao Makuu ya timu ya Azam FC, Chamazi  na leo ameanza mazoezi katika Uwanja wa Azam Comlex chini ya kocha Stewart Hall na muda wowote atasaini mkataba.

 

Wanga mchezaji wa zamani wa El Merrikh ya Sudan aliyoachana nayo baada ya mkataba wake kumalizika ameuambia mtandao huu kuwa amefurahi kuanza kazi na Azam na malengo yake ni kujituma kwa nguvu zote ili timu ifanikiwe.

 

“Nimefurahi kuwa hapa Azam, malengo ni kujituma kwa nguvu ili timu ifikie malengo. Azam ni timu nzuri ina kila kitu, na nimekuwa nikiifuatilia kwa ukaribu imekuwa inasonga mbele kadri siku zinavyokwenda,”alisema Wanga.

 

Akizungumzia kilichomuondoa Sudan, Wanga amesema, alihitaji kubadilisha mazingira baada ya kumaliza mkataba. Maisha ya Sudan ni magumu kwa wageni, kuna joto kali sana, vumbi na utamaduni tofauti. Nilipomaliza mkataba, nilihitaji changamoto mpya. Nashukuru nimeipata Azam FC.

 

Kocha Stewart Hall amesema, amefurahi kumwona Wanga ni mchezaji mzuri lakini anataka kumfahamu zaidi atakapokuwa naye kikosini.