Wachezaji wahiri na maarufu katika ukanda huu wa CECAFA Jean-Baptiste Mugiraneza  Migi toka APR mwenye uwezo wa kucheza nafasi za ulinzi na kiungo pamoja na Mshambulizi Mkenya anayekipiga El Marrekh  ya Sudan Allan Wanga wanatua Azam FC imethibitishwa.

Mazungumzo na Wanga yamefika sehemu nzuri huku Migi ambaye tayari ameichezea Azam FC mechi mbili za kirafiki atasajiliwa lakini atarudi Rwanda kuichezea APR itakayoshiriki mashindano ya Afrika Mashariki CECAFA jijini Dar es Salaam na baada ya hapo atajiunga na Azam FC moja kwa moja.

Wanga mchezaji aliyefunga goli la tatu lililoiondoa Azam FC kwenye mashindano ya klabu bingwa Afrika amekuwa kwenye rada za viongozi wa Azam FC kwa muda mrefu tangia alipofunga goli lililoisaidia Merrikh kutwaa ubingwa wa CECAFA mjini kigali Rwanda. Anajiunga na vijana wa Chamazi baada ya kumaliza mkataba wake wa kuwatumikia matajiri wa kitongoji cha Omduman Khartoum.

Jean-Baptiste Mugiraneza Migi ambaye amekuja nchini na kuungana na kikosi kilichoenda Tanga kushiriki mechi mbili za majaribio na Azam FC amemvutia sana kocha Stewart Hall ambaye ameuagiza uongozi umsajiri haraka iwezekanavyo.

Usajili wa wachezaji hawa unafanya idadi ya wachezaji wapya waliosajiliwa Azam FC msimu huu kufika wanne

Wengine ni wazalendo Ame Ally Zungu toka Mtibwa Sugar na Ramadhan Singano Messi ambaye ni mchezaji huru