Kikosi cha Azam FC kinachojiandaa na mashindano ya Kagame Cup kimeendelea na maandalizi yake kwenye viunga vya Azam Complex huku benchi jipya la ufundi likifurahia vipaji vilivyopo.

 

Wasaidizi wa Stewart toka uingereza na Romania wameonekana kufurahishwa sana na nidhamu, vipaji na kujituma kwa wachezaji waliowakuta Azam FC na wakasema watahakikisha wanatumia maarifa yao yote kuhakikisha wanaifanya Azam FC klabu inayoheshmika Afrika.

 

Wachezaji wa kigeni wameongezea utamu wa mazoezi hayo ambayo wiki iliyopita yalitawaliwa na wachezaji wa kikosi cha vijana (Under 20)

 

Azam FC imekuwa ikifanya mazoezi ya kujenga mwili zaidi kwa kukimbia, Gym, Kuogelea na kuchezea mpira.

 

Kocha Stewart Hall ambaye anafahamika kwa kupenda soka la pasi na kuvutia amemwambia mwandishi wa tovuti hii kuwa amefurahia sana maamuzi ya TFF ya kuongeza wachezaji wa kigeni hadi saba na akasema anahijati kuangalia kikosi alichonacho kabla ya kuamua nani aje kati ya wachezaji ambao wapo kwenye mipango ya Azam FC

 

“kuna mshambuliaji kutoka Zambia, kuna golikipa toka Ivory Coast, kuna kiungo toka Rwanda na wengine kadhaa ambao wapo kwenye mipango yetu. Nafasi ni mbili. Kabla ya kuamua yupi atakuja nahitaji kufanya tathmini ya kina kuangalia ni eneo gani lina mapungufu kasha tuweze kuamua” alisema Stewart Hall, kocha mwenye uzoefu wa kutosha na ligi kuu ya Tanzania.