Azam imeanza rasmi mazoezi leo kwa ajili ya kujiandaa na michuano mbalimbali inayowakabili kama Kombe la Kagame, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho ambapo kocha wao Mkuu Mungereza, Stewat Hall amesisitiza lazima kieleweke safari hii.

 

Stewart ambaye anafurahi kurudi kwenye timu yake hiyo ya zamani aliyoichukua baada ya Mcameroon Joseph Omog kuondolewa, aliingia Uwanjani hapo kwa mikwara akiwa ameambatana na msaidizi wake, Mario Marineca.

 

Ambapo aliongozana Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba kwa ajili ya kumwonyesha mazingira ya eneo hilo kwa sababu ni muda mrefu tangu alipoondoka na alitembelea gym, viwanja vyote,, vyumba vya kupumzikia wachezaji na vyumba vya kulala wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

 

“Nimefurahi kurudi, nataka kuitengeneza Azam mpya kabisa itakayokuwa tishio kwenye michuano mbalimbali na mambo yatakwenda sawa,”alisema Stewart.

 

Jumla ya wachezaji 30 ndiyo waliwasili kwenye mazoezi hayo ambapo kati yao, 21 ni kutoka timu B na 10 wa timu ya wakubwa.

 

Idadi hiyo ni kwa sababu sehemu kubwa ya wachezaji wao wana majukumu kwenye vikosi vya timu ya Taifa Stars, pia wale wa kigeni bado hawajafika isipokuwa Mrundi Didier Kavumbagu peke yake ndiyo amekuwa wa kwanza, alifika jana.

 

Kutoka timu ya wakubwa waliohudhuria mazoezi ni Himid Mao, Abdallah Kheri, Farid Mussa, Said Morad wao walifanya lakini Joseph Kimwaga,Mcha Khamisi na Wazir Salum,  walikuwa na programu maalumu kwa sababu ni majeruhi wakati Kavumbagu hakufanya kwa sababu ya uchovu wa safari.