KOCHA Mcameroon, Joseph Marius Omog leo amepoteza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Voacom Tanzania Bara tangu ajiunge na Azam FC Desemba mwaka jana baada ya mechi 18 bila kufungwa.
Azam leo imefungwa 1-0 na JKT Ruvu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na huo unakuwa mchezo wa kwanza kwa mabinga hao wa Bara kupoteza baada ya mechi 38 ndani ya misimu miwili.
Bao lililovunja rekodi za Omog na Azam leo limefungwa na shambuliaji Samuel Kamuntu dakika ya 44, akimalizia krosi ya Najim Magulu aliyepasiwa na Jabir Aziz. 
Mshambuliaji huyo aliyeingia uwanjani dakika ya 10, kuchukua nafasi ya Iddi Mbaga aliyeumia mapema tu anaifanya JKT ishinde mara ya pili mfululizo katika Ligi Kuu msimu huu, baada ya Jumamosi iliyopita kuichapa Prisons 2-1 na sasa inafikisha pointi saba baada ya kufungwa mechi mbili, sare moja na kushinda mbili.
Azam FC inabaki na pointi zake 10, sawa na Mtibwa Sugar na Yanga SC- maana yake mbio za ubingwa sasa zimepamba moto.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gadiel Michael, Said Mourad, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao/Gudence Mwaikimba dk68, Erasto Nyoni, Didier Kavumbangu, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Farid Mussa/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk51
JKT Ruvu; Jackson Chove, Ramadhani Shamte, Napho Zuberi, Madenge Ramadhani, Mohammed Faki, George Minja, Amos Mgisa/Nashon Naftali dk46, Jabir Azizi, Iddi Mbaga/Samuel Kamuntu dk10, Najim Magulu na Ally Bilal/Emmanuel Pius.

Leave a comment