AZAM FC inaingia kambini leo katika hosteli za Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, kujiadaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Meneja wa Azam FC, Jemadari Said Kazumari amesema timu itaingia kambini jioni ya leo katika hosteli za Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuelekea mchezo huo wa Ngao ya Jamii.
Amesema wachezaji wawili beki Wazuri Salum na mshambuliaji, John Bocco ni majeruhi na hawamo kwenye program za mchezo huo.
“Tuna majeruhi wawili ambao hawatakuwepo kwenye programu ya mchezo wa Ngao ya Jamii, ambao ni beki Waziri Salum na Nahodha wetu, John Bocco,”amesema mshambuliaji huyo wa zamani wa Kariakoo United ya Lindi.
Bocco aliuamia katika mchezo wa Robo Fainali Kombe la Kagame dhidi ya El Merreikh ya Sudan ambao Azam FC ilitolewa kwa penalti baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
Jemadari amesema kwamba, wachezaji wengine wote wapo fiti na wamekuwa wakiendelea na mazoezi Uwanja wa Azam Complex na wanatarajiwa kuingia kambini leo.     
Mabingwa hao wa Tanzania Bara wanaonolewa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog watamenyana na washindi wa pili, Yanga SC walio chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo Jumapili Uwanja wa Taifa
Hii itakuwa mara ya tatu mfululizo, Azam FC kucheza mechi ya Ngao ya Jamii na mara zote ikifungwa kwanza na Simba SC na baadaye na Yanga SC- lakini safari hii kocha Omog anataka kupindua matokeo hayo

Leave a comment