BENKI ya NMB imeingia mkataba wa udhamini wa miaka miwili na klabu bingwa ya soka Tanzania Bara, Azam FC ambao utahusu gharama za usafiri na baadhi za uendeshaji wa timu.
Akizungumza leo makao makuu ya klabu, Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Azam FC Sheikh Said Muhammad Said amesema kwamba mkataba huo unaanza mara moja.
Sheikh Said amesema kwamba wanaishukuru NMB kwa kuwapa Mkataba huo na anaamini utaongeza ufanisi katika klabu yao.
“Tumeupokea kwa furaha Mkataba huu na tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa NMB kwa kuungana nasi,”amesema.
Akifafanua kuhusu Mkataba huo, Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Iddrisa Mohammed ‘Father’ amesema NMB itanufaika kwa kutangazwa kwenye jezi za Azam, mabasi na pia kuweka mabango yao kwenye Uwanja wa Azam Complex.
“Nembo za NMB zitapamba jezi za Azam FC kuanzia mazoezini na kwenye mashindano yote, vyombo vyetu vya usaifiri kadhalika vitawekwa nembo za NMB kama itakavyokuwa kwenye Uwanja wetu a Azam Complex,”amesema Father.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Mark Wiessing amesema mafanikio ya Azam FC ndiyo yaliyowavutia kuingia nao ndoa hiyo. “Mafanikio ya Azam FC katika soka ya Tanzania ndiyo yametuvuta kuingia nao ushirika huu,”amesema.

Leave a comment