KIPA kinda wa miaka 19 wa Uganda, amedaka penalti ya Lionel Saint- Preux na kuipeleka El Merreikh ya Sudan Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya kuitoa Azam FC ya Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Nyamirambo, Kigali, Rwanda- Azam walikosa penalti mbili, nyingine Shomary Kapombe aliyegongesha besela na kutoka nje, wakati Merreikh walikosa moja, ya Nahodha Elbasha Ahmed iliyookolewa na kipa Mwadini Ali.
Penalti za Azam zilifungwa na Aggrey Morris, Didier Kavumbangu na Erasro Nyoni, wakati za Merreikh zilifungwa na Alan Wanga, Magdi Abdelatif, Ayman Said na Ali Gefer.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa wa Kenya, Andrew Otieno, dakika 90 zilimalizika kwa sare ya 0-0, ngome za timu zote zikiwa imara haswa.
John Bocco alikaribia kuifungia Azam dakika ya 26, lakini akashindwa kumalizia pasi nzuri ya Aggrey Morris kwa kupiga nje. Leonel Saint-Preux naye akagongesha mwamba dakika ya 28 baada ya pasi nzuri ya Kipre Tchetche
Amir Kamal wa Merreikh alichelewa kuiunga krosi nzuri ya Nahodha Elbasha Ahmed dakika ya 26 na kipa Mwadini Ali akaiwahi na kuidaka.
Kipindi cha pili, Merreikh walitawala zaidi sehemu ya kiungo, huku Azam wakipitisha mashambulizi yao pembeni zaidi.
Nafasi nzuri zaidi kwa Azam FC kipindi cha pili ilikuja dakika ya 61, baada ya shuti la Kipre Tchetche kupanguliwa na beki wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Magoola.
Kwa Merreikh, Alan Wanga alipoteza nafasi mbili dakika ya 78 na 80, akipiga mashuti makali, moja likitoka sentimita chache na lingine Mwadini Ali akapangua ikawa kona tasa.
Azam FC sasa inarejea Dar es Salaam kujiandaa kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC, Septemba 13 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Marreikh itasubiri mshindi kati ya KCC ya Uganda na Atlabara ya Sudan Kusini.
Hii ni mara ya pili Azam FC kucheza Kombe la Kagame, mara ya kwanza mwaka 2012 ambao iliingia Fainali na kufungwa Yanga SC mabao 2-0. 
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ali, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’/Didier Kavumbangu dk54, Kipre Tchetche na Leonel Saint-Preux.
El Merreikh; Salim Maogola, Elbasha Ahmed, Khamis Bakhiet, Ayman Said, Ali Gefer, Serge Wawa, Alla Eldien, Amir Kamal, Ramadhan Agab/Ragi Abdalate dk69, Mohamed Traore/Magdi Abdeltatif dk87 na Gabir Abdu Mohamed/Alan Wanga dk74.

Leave a comment