AZAM FC imemaliza kwa ushindi mnono mechi za makundi, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya kuifumua mabao 4-1 Adama City ya Ethiopia.
Kwa matokeo hayo Azam FC ya Tanzania Bara, imepanda kileleni mwa Kundi A kwa kufikisha pointi nane baada ya mechi nne, ikishinda mbili na sare mbilihivyo kutinga Robo Fainali kibabe.
Rayon Sport ambayo hivi sasa inacheza na Atlabara ya Sudan Kusini, inaweza kupanda kileleni mwa kundi hilo iwapo itashinda.
Dakika 45 za kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1, Azam wakitangulia kupitia kwa Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ akiunganisha krosi ya Khamis Mcha ‘Vialli’ kabla ya Desaleny Debesh kuisawazishia Adama dakika ya 39.
Refa Mohamed Hassan kutoka Somalia alikataa bao la Kipre Herman Tchetche dakika ya 42, akidai kipa alibughudhiwa na kipindi cha pili Azam iliingia na moto mkali na kufanikiwa kuongeza mabao matatu.
Alianza Didier Kavumbangu dakika ya 55, akimalizia krosi ya Erasto Nyoni akafuatia Khamis Mcha ‘Vialli’ dakika ya 60 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa na Kipre Tchetche akamalizia dakika ya 74, krosi ya Nyoni
Kocha Mcameroon Joseph Marous Omog alifurahia matokeo hayo na akasema sasa anajipanga kwa Robo Fainali.  “Ushindi huu ni mzuri, nafurahi tunaingia Robo Fainali kwa kujiamini, sasa tunaelekeza nguvu zetu huko,”alisema
Kikosi cha Azam FC; Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Gardiel Michael/Said Mourad dk51, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Khamis Mcha ‘Vialli’/Farid Mussa dk61, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Mudathir Yahya dk72, John Bocco ‘Adebayor’, Didier Kavumbangu na Kipre Tchetche.
Adama City; Yakoub Fiseha/Yeraswork Terefe dk38, Suleiman Mohamed, Henok Gemtesa, Demetros Wisilase, Mintesinot Kebede, Wonooson Milkesa, Abreham Yisak, Ameha Belete, Abdulkerim Abafogi, Desaleny Debesh/Abiy Beyene dk68 na Benyam Ayele.

Leave a comment