AZAM FC itamenyana na El Merreikh ya Sudan katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Jumatano Uwanja wa Nyamirambo mjini hapa.
Hiyo inafuatia Atlabara ya Sudan Kusini kufungwa 1-0 na wenyeji, Rayon Sport ya Rwanda katika mchezo wa mwisho wa Kundi A jioni hii Uwanja wa Nyamirambo mjini hapabao pekee la Mutombo Govin dakika ya 87.
Kwa matokeo hayo, Rayon inamaliza kileleni mwa kundi hilo, ikifikisha pointi 10, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi nane, wakati Atlabara inamaliza katika nafasi ya tatu kwa pointi zake, hivyo nayo inakwenda Robo Fainali pia.  
Rayon itamenyana na KCC ya Uganda au APR ya Rwanda pia, itafahamika baada ya mechi za mwisho za Kundi B kesho.  
Mapema katika mchezo wa kwanza wa kundi hilo jioni ya leo, Azam FC iliifumua mabao 4-1 Adama City ya Ethiopia.
Dakika 45 za kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1, Azam wakitangulia kupitia kwa Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ akiunganisha krosi ya Khamis Mcha ‘Vialli’ kabla ya Desaleny Debesh kuisawazishia Adama dakika ya 39.
Refa Mohamed Hassan kutoka Somalia alikataa bao la Kipre Herman Tchetche dakika ya 42, akidai kipa alibughudhiwa na kipindi cha pili Azam iliingia na moto mkali na kufanikiwa kuongeza mabao matatu.
Alianza Didier Kavumbangu dakika ya 55, akimalizia krosi ya Erasto Nyoni akafuatia Khamis Mcha ‘Vialli’ dakika ya 60 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa na Kipre Tchetche akamalizia dakika ya 74, krosi ya Nyoni
Azam FC sasa itamenyana na mshindi wa pili wa Kundi B, El Merreikh ya Sudan katika Robo Fainali Agosti 20, Uwanja wa Nyamirambo.

Leave a comment