AZAM FC kesho itacheza mechi yake ya mwisho ya Kundi A, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Adama City ya Ethiopia bila beki aliye katika kiwango cha juu hivi sasa, Shomary Kapombe.
Mchezaji huyo wa zamani wa AS Cannes ya Ufaransa na Simba SC ya Tanzania pia, anasumbuliwa na nyama za paja na siku ya pili leo ameshindwa kufanya mazoezi na wenzake.
Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog amesema mbali na Kapombe, mshambuliaji Mhaiti, Leonel Saint- Preux ambaye pia yupo vizuri, naye atakosekanawote wakiwa wanasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
Beki Waziri Salum anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu wakati kiungo Himid Mao ana kadi mbili za njano naye hatacheza.   
Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyekosa mechi ya sare ya 2-2 na Atlabara ya Sudan Kusini, amefanya mazoezi jana na leomaana yake kesho anaweza kurudi uwanjani.
Azam FC inahitaji ushindi kesho ili kuongoza Kundi A iweze kupata mpinzani nafuu katika Robo Fainali. Wenyeji Rayon Sport ambao watamaliza na Atlabara wanaongoza kundi hilo kwa sasa kwa pointi zao saba, wakati Azam ina pointi tano.
Atlabara yenye pointi tatu na Adama pointi mbili, zote zinataka kushinda kesho Uwanja wa Nyamirambo ili kuchukua nafasi ya tatu katika kundi hilo, ziweze kuungana na Azam na Rayon kwenda Robo Fainali.  

Leave a comment