KIUNGO Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ wameshindwa kufanya mazoezi na timu yao leo, Azam FC kutokana na kusumbuliwa na maumivu.
Azam baada ya kushinda mechi ya kwanza katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame jana mabao 4-0 dhidi ya KMKM ya Zanzibar, leo imeendelea na mazoezi mjini hapa.
Wakati wachezaji wote wakifanya mazoezi Uwanja wa Kiyovu, eneo la Nyamirambo mjini hapa, Sure Boy na Bocco walikuwa nje wakiugulia maumivu yao.
Sure Boy anasumbuliwa na maumivu ya mguu aliyoyapata jana katika mechi ya pili ya Kundi B na KMKM Uwanja wa Amahoro, wakati Bocco aliumia chini ya goti.
Kocha Joseph Marius Omog, raia wa Cameroon aliamua kuwapumzisha wachezaji hao ili wapate ahueni wakati timu ikijiandaa na mchezo wa tatu wa kundi lake dhidi ya Atlabara ya Sudan Kusini kesho.
“Si maumivu makubwa sana, nadhani baada ya mapumziko ya leo kesho wanaweza kuwa fiti, lakini naangalia uwezekano wa kuwapumzisha zaidi,”alisema Omog.
Azam FC imevuna pointi nne katika mechi mbili baada ya sare ya bila kufungana katika mchezo wa kwanza dhidi ya Rayon Sport na sasa inaongoza Kundi A, ikifuatiwa na wenyeji hao wenye pointi nne pia, KMKM na Atlabara zina pointi moja kila moja, wakati Adamma City ya Ethiopia haina kitu.
Azam FC itakuwa imejihakikishia kwenda Robo Fainali ya michuano ya mwaka huu iwapo itashinda mchezo wa kesho dhidi ya timu hiyo ya Sudan Kusini.
Kocha Omog amesema wachezaji wengine wote wako fiti kuelekea mchezo huo na ana matumaini ya kufanya vizuri.

Leave a comment