MSAFARA wa mwisho wa Azam FC umewasili mjini Kigali, Rwanda jioni hii kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame.
Msafara wa kwanza wa Azam FC uliingia mjini Kigali Alhamisi na jana ukacheza mechi ya kwanza na kutoa sare ya bila kufungana na wenyeji Rayon.
Msafara uliowasili leo ulikuwa na wachezaji watano, ambao ni Eraso Nyoni, Bryson Raphael, Leonel Saint-Preux, Gaudence Mwaikimba na Ismaila Diara.
Kiungo chipukizi Kevin Friday amebaki Dar es Salaam na atakuja na Katibu, Nassor Idrissa ‘Father’ Ijumaa
Kiungo Mhaiti, Joseph Peterson ambaye awali jina lake lilipelekwa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ili acheze mashindano hayo, sasa kuna uwezekano asicheze kutokana na kutokamilisha taratibu za usajili na amebaki Dar es Salaam.   
Mbali na wachezaji waliowasili leo, katika msafara huo walikuwepo na viongozi Abubakar Mapwisa (Utawala), Jamal Bakhresa (Bodi), Iddi Cheche (Benchi la Ufundi), Dk Twalib Mbarak (Tiba), Patrick Kahemele (Utawala) na Joseph Nzawila (Benchi la Ufundi). 
Kikosi ambacho kilitangulia Kigali, mbali na makocha Joseph Marius Omog, Ibrahim Shikanda na Idd Abubakar na Meneja Jemadari Said ni wachezaji makipa; Aishi Manula, Mwadini Ally, mabeki Waziri Salum, Gadiel Michael, Shomary Kapombe, Abdallah Kheri, Aggrey Morris, Said Mourad na David Mwantika.
Viungo Kipre Balou kutoka Ivory Coast, Salum Abubakar, Mudathir Yahya, Himid Mao, Khamis Mcha ‘Vialli’ na Farid Mussa, wakati washambuliaji ni Mrundi Didier Kavumbangu, Leonel Saint- Preux wa Haiti, Kipre Herman Tchetche wa Ivory Coast na John Bocco ‘Adebayor’.
Kikosi kilichotoa sare na Rayon jana kilikuwa; Mwadini, Kapombe, Gardiel, Mwantika, Morris, Kipre Balou, Mao/Mudathir dk89, Sure Boy, John Bocco, Kipre Tchetche na Mcha /Kavumbangu dk70.
Azam FC, mabingwa wa Tanzania Bara, wapo Kundi A pamoja na wenyeji, Rayon Sport, Adamma ya Ethiopia, Atlabara ya Sudan Kusini na KMKM ya Zanzibar.
Kundi B lina timu za APR ya Rwanda, KCC ya Uganda, Atletico ya Burundi, Gor Mahia ya Kenya na Telecom ya Djibouti wakati Kundi C linaongozwa na mabingwa watetezi, Vital’O ya Burundi, El Merreikh ya Sudan, Polisi ya Rwanda na Benadir ya Somalia.
Baada ya sare ya jana na Rayon, Azam itashuka tena dimbani kesho (Agosti 10) kumenyana na jirani zao KMKM, kabla ya kucheza na Atlabara Agosti 12 na kukamilisha mechi za kundi lake, kwa kumenyana na Adamma ya Ethiopia Agosti 16.
Ikumbukwe timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, imechukua nafasi ya Yanga SC katika michuano ya mwaka huu ambao wameondolewa na CECAFA kwa kukiuka kanuni za mashindano.
Yanga SC ilitaka kupeleka kikosi cha pili badala ya kikosi cha kwanza, jambo ambalo walikataliwa na CECAFA.

Leave a comment