MSHAMBULIAJI Ismaila Diara kutoka Mali ameendelea kufanya vizuri zaidi ya wachezaji wenzake wapya wa kigeni kwa kufunga mabao Azam FC.
Azam FC imesajili washambuliaji wapya watatu wa kigeni, Didier Kavumbangu kutoka Burundi, Leonel Saint-Ptreux kutoka Haiti na Diara wanaoungana na Kipre Herman Tchetche wa Ivory Coast, kinara wa mabao wa timu hiyo kwa misimu miwili iliyopita.
Diara jana alifikisha jumla ya mabao matatu aliyoifungia Azam FC katika michezo mitatu ya kujipima nguvu aliyoichezea akifunga bao moja katika ushindi wa 2-1 dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza, Friends Rangers.
Bao lingine la Azam FC, lilifungwa na Gaudence Mwaikimba wakati bao la kufutia machozi la Rangers lilifungwa na Yussuf Mgwao.
Awali, Diara aliifungia Azam FC mabao mawili katika ushindi wa 3-2 dhidi ya kombaini ya Jeshi, bao lingine likifungwa na Mudathir Yahya.
Leonel ana bao moja tu alilofunga dhidi ya Polisi Morogoro katika ushindi wa 1-0, wakati Kavumbangu ana bao moja pia alilofunga katika ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Ruvu, bao lingine likifungwa na Kipre Tchetche.
Azam FC leo itaendelea na mazoezi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam wakati kesho itacheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja huo.

Leave a comment