AZAM FC imeshinda mechi ya tatu mfululizo ya kirafiki, baada ya jana kuilaza mabao 2-1 JKT Ruvu Stars Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, wachezaji wa kigeni wakiendelea kuibeba timu.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, walikwenda kupumzika wakiwa tayari wanaongoza tayari kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Mrundi Didier Kavumbangu na Kipre Tchetche kutoka Ivory Coast.
Kipindi cha pili, kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog alibadilisha karibu wachezaji wote walioanza na JKT Ruvu ya Freddy Felix Minziro ilitumia mwanya huo kujipatia bao la kusawazisha lililofungwa na Hassan Bilal, aliyemalizia kazi nzuri ya Betram Mombeki.
Mshambuliaji mpya wa Azam FC kutoka Haiti, Leonel Saint- Preux alicheza vizuri na ndiye aliyetoa pasi ya bao la pili, wakati Ismaila Diara kutoka Mali alikuwa jukwaani kabisa kutokana na mejeruhi.
Chipukizi waliopandishwa kutoka akademi, Abdul Mgaya, Bryson Raphael, Malik Farid, Dizana Issa na Mudathir Yahya ambao walianza kipindi cha kwanza, wote walicheza vizuri.
Awali, Azam FC ilizifunga kombaini ya Jeshi 3-2, mabao yake yakifungwa Ismaila Diara mawili na Mudathir Yahya moja, kabla ya kuilaza Polisi Morogoro 1-0, bao pekee la Leonel Saint- Preux.

Leave a comment