MSHAMBULIAJI Kipre Herman Tchetche wiki hii amezima uzushi kwamba yuko kwenye mpango wa kuhamia Yanga SC, baada ya kuibukia kwenye mazoezi ya timu yake, Azam FC.
Nyota huyo kutoka Ivory Coast aliwasili mwishoni mwa wiki Dar es Salaam kutoka kwao Abidjan alipokwenda kwa mapumziko baada ya msimu na mwanzoni mwa wiki akaibuka mazoezini Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Kipre alilakiwa na kocha Mcameroon Joseph Marius Omog na kuzungumza naye kwa dakika kadhaa kabla ya kujiunga na wenzake kwa mazoezi.
Baadaye, Kipre alikabidhiwa tuzo yake ya Mchezaji Bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Meneja wa timu hiyo Jemadari Said Kazumari.
Kipre alikuwa amekwishakwenda kwao wakati wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom Tanzania wanakabidhi tuzo za washindi mwezi uliopita
Akizungumza baada ya mazoezi, Kipre alisema kwamba hajawahi hata kufanya mazungumzo na Yanga SC na anashangazwa na habari hizo. “Mimi sijawahi kuzungumza na mtu yeyote wa Yanga, nashangaa sana,”alisema.
Baada ya Azam FC kusajili wachezaji wawili kwa mpigo wa Yanga SC, kiungo Frank Domayo na mshambuliaji Mrundi, Didier Kavumbangu, ikadaiwa klabu hiyo ya Jangwani inataka kulipa kisasi kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu kwa kuwachukua Kipre Tchetche na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’. 
Tayari Sure Boy alikwishakanusha uvumi huo na kusema yeye ana mkataba na Azam na kwa sasa akili yake imelalia kwenye klabu hiyo inayomilikiwa na bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake.

Leave a comment