AZAM FC imelazimika kwenda kumfanyia matibabu ya nyama za paja kiungo Frank Domayo iliyemsajili miezi miwili iliyopita kutoka Yanga SC ya Dar es Salaam.
Domayo amekuwa akicheza na majeruhi bila kujijua, lakini baada ya kusajiliwa Azam FC na kwenda kufanyiwa vipimo vya afya, ikagundulika msuli wake mmoja wa paja umechanika.
Azam FC ikampandisha ndege hadi Afrika Kusini kwenda kwa mtaalamu kufanyiwa upasuaji wa kina, zoezi ambalo limekamilika salama.
“Domayo alikuwa anajitaharisha kufupisha maisha yake ya uwanjani, wataalamu wamesema, kama angeendelea kucheza, msuli mwingine ukakatika, maana yake asingepona na huo ungekuwa mwisho wake wa kucheza soka,”alisema Katibu wa Azam FC, Nassor Idirsa ‘Father’.
Domayo sasa anatarajiwa kuwa nje ya Uwanja kwa miezi miwili, kabla ya kurejea kazini akiwa fiti kabisa.
Aidha, kiungo chipukizi wa Azam FC, Patrick Kimwaga naye amefanyiwa upasuaji wa goti lililokuwa linamsumbua.
“Wachezaji wote hawa wamefanyiwa upasuaji Afrika Kusini na watarejea nyumbani pamoja kuendelea na matibabu, hadi hapo watakapokuwa fiti na kurudi uwanjani,”alisema Father. 

Leave a comment