TIMU ya Azam FC juzi imeanza mazoezi kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Meneja wa Azam FC, Jemadari Said Kazumari amesema leo kwamba wachezaji wote walio kwenye mipango ya msimu ujao walifika mazoezini, kasoro watatu wa kigeni.
Amewataja wachezaji hao wa kigeni kuwa ni Kipre Tchetche anayetarajiwa kuwasili leo, mdogo wake Kipre Balou wote kutoka Ivory Coast anayetarajiwa kuwasili Juni 26 na Ismaila Diara wa Mali anayetarajiwa kutua kesho.
Jemadari amesema kwamba wachezaji wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars walifika siku ya kwanza juzi, lakini jana wakaruhusiwa.
“Tumewaruhusu kwa sababu wana safari na timu ya taifa, sasa wamekwenda kujiandaa, lakini wengine wote waliobaki tupo nao hapa na mambo yanaendelea vizuri,”alisema.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa zamani wa Kariakoo United ya Lindi, alisema kwamba kwa sasa mazoezi hayo yanasimamiwa na kocha Msaidizi, Muingereza Kali Ongala.
Amesema kocha Mkuu, Mcameroon Joseph Marius Omog anatarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo.
Azam FC ambao ndiyo mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Bara, pamoja na jukumu la kutetea taji lao hilo msimu ujao, lakini mwakani pia watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.

Leave a comment