Mfungaji wa bao la tatu la Azam hana, Kipre Tchetche kushoto akishangilia na David Mwantika kulia
 
KOCHA Mcameroon wa Azam FC amewashukuru wachezaji wake kwa kazi nzuri waliyoifanya jana Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani timu hiyo ikishinda mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, lakini amewaambia; “tunahitaji pointi sita zaidi”.
Akizungumza baada ya mechi ya jana, Mcameroon huyo alisema; “Ni furaha. Ni ushindi mzuri, tumevuka kikwazo kimoja, vijana waliuanza mchezo vizuri wakizingatia nilichowaambia. Karibu kila mmoja alitekeleza majukumu yake vizuri. Wapinzani walikuwa wagumu, lakini tumechukua pointi tatu,”alisema.
Omog alisema anajivunia wachezaji wake na hana cha kuwaambia zaidi ya asante pamoja kama timu na akawataka kuendeleza mshikamano huo daima. Hata hivyo, Omog amewaambia wachezaji wake kwamba wanahitaji kushinda pia mechi mbili za mwisho ili wamalize ligi vizuri.
Ushindi wa jana umeifanya Azam FC ifikishe pointi 56 baada ya kucheza mechi 24 na kujivuta karibu kabisa na chumba kinachohifadhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu, ikiwaacha kwa pointi nne mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 52 za mechi 24 pia.
Jumapili, timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake itasafiri hadi Mbeya kumenyana na wenyeji, Mbeya City katika mchezo ambao ikishinda itajihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu, kabla ya kucheza mechi ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu Aprili 19, Uwanja wake wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. 

Leave a comment