AZAM FC imejisogeza karibu na ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni hii kuilaza Simba SC kwa mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Azam itimize pointi 53 baada ya mechi 23, wakati Yanga SC iliyofungwa 2-1 na Mgambo JT leo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga inabaki na pointi zake 46 baada ya mechi 22.
Shukrani kwake mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga bao la ushindi dakika ya 56 kwa kichwa kufuatia pasi ya tika tak ya Kipre Herman Tchetche
Tayari timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1 hadi mapumziko, Azam FC wakitangulia kupata bao lao kupitia kwa Khamis Mcha Vialli dakika ya 16 na Simba SC wakisawazisha kupitia kwa Joseph Owino dakika ya 45 na ushei.
Mcha alifunga bao kwa urahisi baada ya kutengewa mpira kwa kifua na Kipre Tchetche aliyepokea krosi Gardiel Michael- ambaye naye alipata pasi ya John Bocco aliyefanya kazi kubwa ya kupanda na mpira kutokea nyuma.
Owino alifunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na winga machachari, Ramadhani Singano ‘Messi’.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Henry Joseph/Abdulhalim Humud dk66, Haruna Chanongo, Amisi Tambwe, Uhuru Suleiman na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Aggrey Morris, David Mwantika, Kipre Balou, Himid Mao/Bryson Raphael dk75 , Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’, Kipre Tchetche/Brian Umony dk80 na Khamis Mcha ‘Vialli’/Kevin Friday dk55.

Leave a comment