Msafara wa timu ya Azam upo katika hali nzuri hapa Beira Msumbiji ukijiandaa na mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa Jumapili hii dhidi ya wenyeji Ferroviario da Beira.

 

Ujumbe mzima unaojumuisha watu 39 wakiwemo wachezaji 21, viongozi wa jopo la ufundi na maofisa wengine umefikia katika hoteli ya Rainbow Mozambique iliyopo Mtaa wa Bagamoyo hapa Beira ambayo ni hadhi ya nyota tatu.

 

Safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Beira ilikamilika majira ya saa 1 usiku kwa saa za Msumbiji (Saa 2 usiku Tanzania) jana Jumatano baada ya kuunganisha ndege Johannesburg Afrika Kusini na kuruka kwa muda wa saa mbili hadi Beira. Mapema safari ya Dar es Salaam hadi Afrika Kusini ilichukua saa 3. Wachezaji wote wako katika hali nzuri kiafya na kisaiklojia

 

 Asubuhi leo timu imefanya mazoezi ya kwanza tangu kuwasili kwenye uwanja unaomilikiwa na klabu mwenyeji katika harakati za kusaka matokeo mazuri kuelekea hatua ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho.

 

Azam inahitaji ushindi au sare ili iweze kusonga mbele kufuatia ushindi wa nyumbani wa 1-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Azam Complex Dar es Slaam Jumapili iliyopita.

 

Ikiwa itafaulu kuwatoa Ferroviarrio Azam itapambana na washindi wa pili wa ligi ya Zambia, Zesco mwishoni mwanzoni mwa mwezi Machi.