Azam wamekalia usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya  Yanga kulazimishwa sare 0-0 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Azam wamekalia uongozi ligi hiyo baada ya kuichapa Rhino Rangers kwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi, na kufikisha pointi 33, huku Yanga wakiwa na  pointi 32 na Mbeya City (31) wakibaki nafasi ya tatu baada ya kulazimishwa sare 1-1 na Ruvu Shooting.

Mshambuliaji Kipre Tchetche ameendelea kuibeba Azam baada ya kuifungia bao pekee dakika 26, kwa shuti kali la mguu wa kushoto akiunganisha pasi ya Mohamed Kone.

Tchetche amefikisha mabao tisa hadi sasa akiwa nyuma kwa bao moja kwa kinara wa ufungaji Amisi Tambwe wa Simba mwenye magoli 10.

Tanga; Mabingwa watetezi Yanga, watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kutumia nafasi nyingi  walizozipata katika kipindi cha kwanza baada ya kupata kona sita katika dakika 30 za kwanza kabla ya wenyeji Coastal Union kuamka.

Kiungo Haruna Niyonzima alikosa bao baada ya shuti lake kudakwa na Shaabani Kado dakika 12, mashabiki wa Yanga dakika 29 walirusha chupa za maji uwanjani kupinga uamuzi wa mwamuzi wa mchezo huo, Simon Mbelwa, Pwani.

Wenyeji Coastal Union waliamka dakika ya 30, na kuanza kushambulia, lakini mashuti ya Yayo Lutimba, Haruna Moshi na Kenneth Masumbuko yaliokolewa kwa ustadi mkubwa na kipa Deo Munishi wa Yanga.

Mlandizi, Wenyeji Ruvu Shooting wameipunguza kasi Mbeya City baada ya kuilazimisha sare 1-1 kwenye Uwanja wa Mabatini

Shooting walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia Jerome Lembele dakika 4, kabla ya City kusawazisha kupitia Deus Kaseke dakika 14.

Kagera Sugar wameendelea kusuasua baada ya kulazimisha sare 0-0 na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Kaitaba.

Mashabiki Yanga wapata ajali Tanga

Mashabiki wanaodhaniwa wa Yanga, wamepata ajali wakiwa safarini kuelekea mkoani Tanga kuishangilia timu yao ikivaana na Coastal Union.

Habari hii ni kwa hisani ya gazeti la Mwananchi