Brian Umony na Himid Mao jana waliifungia Azam FC magoli na kuifanya ianze kwa ushindi wa 2-0 kwenye mashindano ya Mapinduzi Cup yanayorushwa moja kwa moja na Azam TV

Brian Umony aliyeingia dakika ya 59 kuchukua nafasi ya Muamad Ismael Kone, alicheza vizui sana na kusaidia kupatikana kwa ushindi huo

Himid Mao aliifungia Azam bao la pili dakika ya 86, baada ya kuuwahi mpira uliokuwa unaelekea mikononi mwa kipa Silima kufuatia shuti la Salum Abubakar na kupiga shuti lililotinga nyavuni.

Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Mfaume Ali, mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mcameroon Joseph Marius Omog kipindi cha pili kuwatoa Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre Herman Tchetche na Kone na kuwaingiza Umony, Joseph Kimwaga na Seif Abdallah ndiyo yalileta ushindi huo.    

 

Azam walitawala zaidi mchezo katika dakika 45 za kwanza, lakini wakakosa mbinu za kuivunja ngome ya Spice, inayoundwa na wachezaji mchanganyiko wa Unguja.

Kocha Omog alifanya mabadiliko kwenye kikosi cha kwanza cha Azam leo, akimrejesha Himid Mao kucheza nafasi ya kiungo pamoja na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Kipre Michael Balou, huku Erasto Nyoni akicheza beki ya kulia na Waziri Salum beki ya kushoto.

Azam ilitawala sehemu ya kiungo na pasi nyingi ziliwafikia washambuliaji Kipre Herman Tchetche na Muamad Ismael Kone, lakini wakashindwa kabisa kufunga kipindi cha kwanza.

Kwa ushindi huo, Azam inaongoza Kundi C kwa pointi zake tatu, na kubaki au kushuka itategemea na matokeo ya mchezo wa pili jioni ya leo Uwanja wa Amaan kati ya Ashanti United ya Dar es Salaam na Tusker FC ya Kenya.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ali, Erato Nyoni, Waziri Salum, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakar, Muamad Kone/Brian Umony dk59, Kipre Tchetche/Seif Abdallah dk 70 na Khamis Mcha ‘Vialli/Joseph Kimwaga dk46