AZAM FC leo imemkaribisha kocha wake kwa zawadi ya Krismass baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo wa kirafiki wa kujaribu mfumo wa tiketi za elekroniki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni hii.

 

Hadi mapumziko, tayari Azam FC, walio chini ya kocha mpya Mcameroon, Joseph Marius Omog ambaye anataka timu imiliki mpira mwanzo mwisho walikuwa mbele kwa mabao 2-0.

 

Brian Omony alitangulia kuifungia Azam Fc bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 10 kazi nzuri Mganda, nahodha John Bocco, Aggrey Morris na Said Moradi.

 

Umony sasa anaonekana kurudi katika kasi yake ya mchezo baada ya kuandamwa na majeruhi msimu uliopita

 

Bao la pili liliwekwa nyavuni kwa mkwaju wa penalti na mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 30, baada ya Ayoub Kitala kuurudisha kwa mkono mpira uliokuwa unaelekea nyavuni. Baada ya Bocco kuukwamisha mpira nyavuni.

 

Refa Israel Mujuni Nkongo alimpa kadi nyekundu beki wa Ruvu na kuifanya timu ya Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ imalizie dakika 50 za pambano hilo ikiwa pungufu.

 

Mchezo ulikuwa mzuri kipindi cha kwanza timu zote zikicheza soka ya kufundishwa na makocha waliosomea Ujerumani, Mkwasa wa Ruvu na Omog wa Azam FC.

 

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko karibu ya vikosi vizima na aliyekuwa kivutio katika ngwe hiyo ni mshambuliaji mpya kutoka Ivory Coast Muamad Ismael Kone toka Ivory Coast aliyeingia pia kwa upande wa Azam FC. 

 

Kone alionyesha uwezo mkubwa sana wa kucheza soka na akafunga bao zuri la tatu dakika ya 57.

Baada ya mechi hiyo, Azam inatarajiwa kwenda Zanzibar kutetea Kombe la Mapinduzi, michuano inayoanza mapema Januari 1, mwakani, wakati Ruvu itaendelea na maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

 

Baada ya Mchezo kocha Omog alisema ana kazi kubwa ya kufanya kwani timu inapoteza mipira kirahisa, haina kasi na inapopoteza mipira wachezaji wanategeana kukaba

 

Alisifia kikosi cha Azam FC kuwa kina wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu na akasema hadi utakapofika muda wa kucheza michezo ya kimtaifa anadhani timu itakuwa tayari