Ushindi wa 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting Stars umeiwezesha Azam FC kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi kuu Tanzania bara ikiwa imesalia na mchezo mmoja kumaliza mzunguko wa kwanza wa msimu huu wa 2013-2014.

 

Azam FC imepata ushindi huo na kufikisha pointi 26 sawa na Mbeya City ya mkoani Mbeya zikitofautiana kwa idadi ya magoli huku timu zote zikiwa hazijapoteza hata mchezo mmoja, kwa matokeo ya jana timu ya Yanga inashuka hadi nafasi ya tatu.

 

Mbeya City na Azam FC zitakutana katika mchezo wao wa mwisho wa kukamilisha hatua ya mzunguko wa kwanza, mchezo ambao kila timu itahitaji kushinda ili isiharibu rekodi yake pamoja na kuendelea kuongoza kwenye msimamo wa ligi kuu, mechi hiyo itachezwa Nov 7 kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi na kurushwa moja kwa moja na Azam TV kupitia Chanel 10.

 

Katika mchezo wa huo uliozikutanisha Azam FC na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Azam Complex, Azam FC waliandika bao la kwanza mapema katika dakika ya kwanza ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji Kipre Tchetche aliyeunganisha vizuri mpira wa  Joseph Kimwaga.

 

Azam FC ikiongoza 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, ilipata goli la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza katika dakika ya 45, goli lililofungwa na mshambuliaji chipukizi Kimwaga kwa kichwa akimalizia mpira wa mwisho uliopigwa na Waziri Salum na kupeleka timu zote mapumziko Azam FC wakiongoza 2 huku Ruvu wakiwa hawajapata kitu.

 

Kipindi cha pili timu zote ziliingia kwa kasi Azam FC walifanya mabadiliko dakika ya 60 alitoka nahodha Himid Mao nafasi yake ikachukuliwa na Jabir Aziz na dk 68 aliingia Farid Maliki kuchukua nafasi ya Kimwaga mabadiliko hayo yaliisaidia Azam FC kupata goli la tatu katika dakika ya 70 kupitia kwa Khamis Mcha aliyetumia vyema uzembe wa beki ya Ruvu na kumalizia mpira wa Kipre, goli hilo lilimaliza mchezo Azam FC wakiondoka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting.

 

Kipre amefikisha jumla ya magoli saba ya kufunga huku Kimwaga na Mcha wakifikisha magoli mawili kila mmoja.

 

Ruvu Shooting watajutia nafasi za wazi walizokosa katika nyakati tofauti wachezaji Hassan Dilunga, Cosmas Lewis, Elius Maguli na Said Dilunga walijaribu kupiga mashuti lakini yakaokolewa na kipa Mwadini Ally wa Azam FC na mengine kutoka nje hivyo kumaliza mchezo wakiwa hawajaziona nyavu za Azam FC.

 

Azam FC: Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Said Morad, Aggrey Moris, Kipre Bolou, Joseph Kimwaga/Farid Maliki 68’, Himid Mao/Jabir Aziz 60’, Kipre Tchetche, Humphrey Mieno/Kelvin Friday 83’ na Khamis Mcha.

 

Ruvu Shooting: Abdul Juma, Michael Aidan, Stephano Mwasyika, Mangasini Mbonosi, Shaaban Sunza, Juma Seif Dion, Juma Nade, Hassan Dilunga, Said Dilunga, Elias Maguli na Cosmas Lewis/Raphael Kiara.