Magoli mawili ya mshambuliaji Tchetche Herman Kipre wa Azam FC yameipa pointi tatu muhimu timu hiyo na kubaki kileleni mwa ligi kuu baada ya kuifunga Simba SC 2-1 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom (VPL) uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameifikisha Azam FC kuwa na pointi 23 ikiongoza huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote katika msimu huu wa 2013/2014, Simba wamebaki na pointi zao 20 na kuwa ya pili katika msimamo wa ligi kuu.

Katika mchezo huo Azam FC ilimuanzisha kwa mara ya kwanza mshambuliaji wake chipukizi Joseph Kimwaga ambaye alionyesha uwezo wake kwa kutengeneza nafasi nyingi lakini hazikuweza kuzaa matunda.

Simba SC walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 21 likifungwa na mshambuliaji mwenye kasi Ramadhan Singano aliyemalizia mpira uliopigwa na Zahor Pazi na kubadili matokeo Simba ikiongoza 1-0 dhidi ya Azam FC.

Dakika moja kabla ya kwenda mapumziko Kipre aliiandikia Azam FC goli la kusawazisha kwa shuti akiunganisha mpira uliochongwa vizuri na beki Erasto Nyoni, goli hilo lilizipeleka timu zote mapumziko zikiwa zimefungana 1-1.

Kipindi cha pili Azam FC walianza kwa mabadiliko walitoka Joseph Kimwaga na Said Morad ambao walifanya kazi nzuri katika kipindi cha kwanza nafasi zao zikachukuliwa na Farid Mussa Maliki na David Mwantika.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwa Azam FC ambao dakika ya 71 walipata goli la pili na la ushindi lililowekwa wavuni na Kipre akiwatoka mabeki wa Simba na kufunga goli hilo lililomaliza mchezo Azam FC wakitoka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba SC.

Azam FC itaingia tena katika maandalizi kwa ajili ya mchezo wao mwingine wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting utakaochezwa siku ya Alhamis kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

Azam FC: Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Said Morad/David MwantikaWaziri Salum, Aggrey Morris, Michael Bolou, Tchetche Kipre, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco, Humphrey Mieno/Khamis Mcha na Joseph Kimwaga/Farid Mussa Maliki.

Simba SC: Abel Dhaira, William Lucian, Issa Rashid, Hassan Khatib, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhan Singano, Said Ndemla, Betram Mombeki, Zahor Pazi na Amri Kiemba.