Timu ya Azam FC imeendelea kung’ang’ania katika nafasi  ya pili katika msimamo wa ligi kuu baada ya kupata ushindi mwingine kwa kuifunga JKT Ruvu Stars jumla ya magoli 3-0,kwenye mchezo wa ligi kuu uliochezwa Uwanja Azam Complex jijini Dar es Salaam.

 

Matokeo hayo yameoingeza pointi tatu Azam FC na kufikisha pointi 17 ikiwa nafasi ya pili huku Simba ikiongoza ligi kwa kufikisha pointi 18.

 

Katika mchezo huo Azam FC iliwatumia wachezaji wake wawili kutoka kikosi chake cha Azam Academy ambao ni Faridi Maliki na Joseph Kimwaga ambao kwa nyakati tofauti wameongeza nguvu katika timu hiyo.

 

Goli la kwanza kwa Azam FC liliwekwa wavuni dk 16 ya mchezo huo kupitia kwa Humphrey Mieno aliyemalizia mpira uliopigwa na Faridi Maliki na kubadili kibao cha matokeo na kuwa Azam FC 1-0 JKT Ruvu Stars.

 

Kabla ya kumaliza kipindi cha kwanza mlinzi Erasto Nyoni aliifungia Azam FC bao la pili kwa kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Waziri Salum, na kupeleka timu hizo mapumziko Azam FC ikiwa mbele kwa 2-0 dhidi ya JKT Ruvu.

 

Kipindi cha pili kilianza na kasi kwa JKT Ruvu ambao walionekana kufanya mashambulizi mengi tofauti na kipindi cha kwanza, walifanya mabadiliko kuimarisha kikosi chao walitoka Salum Machaku, Paul Ndauka na Sostenes Manyasi nafasi zao zikachukuliwa na Amos Mgisa, Bakari Kondo na Hussein Bunu.

 

Azam walitumia kipindi cha pili vizuri kwa kufanya mabadiliko waliingia Joseph Kimwaga, Himid Mao na Khamis Mcha kuchukua nafasi za Farid Maliki, Humphrey Mieno na Kipre Tchetche mabadiliko hayo yaliiwezesha Azam FC kufanya mashambulizi mengi kuliko JKT Ruvu.

 

Dakika ya 90 kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alikamilisha idadi ya magoli kwa kuifungia Azam FC bao la tatu kwa shuti la pembeni baada ya kuweza kumtoka beki na nahodha wa JKT Ruvu, Damas Makwaya na kumaliza mchezo Azam FC ikitoka na ushindi mnono wa 3-0 dhidi ya JKT Ruvu.

 

Kwa matokeo hayo Azam FC imecheza jumla ya mechi 9 bila kupoteza mchezo wowote ikiwa sawa na Mbeya City huku Simba ikicheza mechi 8 bila kufungwa.

 

Azam FC itaingia kambini kujiandaa na mchezo mwingine wa ligi kuu dhidi ya Oljoro  JKT utakaochezwa Jumamosi ya Octoba 19, katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

 

Azam FC: Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Aggrey Moris, Said Morad, Michael Bolou, Tchetche Kipre/Khamis Mcha Viali, Salum Abubakar, John Bocco, Humphrey Mieno/Himid Mao, Farid Maliki/Joseph Kimwaga.

JKT Ruvu:Hamis Seif, Mussa Zuberi, Stanley Nkomola, Damas Makwaya, Jamal Said, Nashon Naftari, Sostenes Manyasi/Hussein Bunu, Haruna Adolf, Paul Ndauka/Bakari Kondo, Salum Machaku/Amos Mgisa na Emmanuel Pius.