Timu ya Azam FC imesogea hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu ya Vodacom (VPL) baada ya kuifunga Mgambo JKT 2-0, kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

 

Azam FC imepata ushindi huo na kufikisha jumla ya pointi 14 ikiwa nyuma ya Simba SC inayoongoza ligi kwa kuwa na pointi 15, Mgambo wao wanabaki nafasi ya pili kutoka chini wakiwa na pointi zao 5.

 

Katika mchezo huo kipindi cha kwanza timu zote zilitoshana nguvu kwa kutokufungana huku kila timu ikifanya mashambulizi, dk 26 John Bocco aliyekuwa nahodha wa Azam FC alikosa goli la wazi baada ya kupiga nje mpira akiwa yeye na lango la Mgambo.

 

Azam FC walizidi kulisakama lango la Mgambo, dk 31 na 45 Kipre Tchetche alijaribu kwa kupiga mashuti lakini yakaokolewa na kipa Tony Kavishe wa Mgambo, Mgambo nao hawakuwa nyuma dk 32 Salum Gilla alipiga mpira wa mbali ikadakwa vizuri na kipa Mwadini Ally wa Azam FC.

 

Kipindi cha pili kilikuwa kizuri kwa Azam FC ambao walianza kwa kufanya mabadiliko dakika 45 alitoka Brian Umony nafasi yake ikachukuliwa na mchezaji chipukizi Farid Mussa Maliki aliyeongeza kasi ya mashambulizi upande wa Azam FC.

 

Mabadiliko hayo yalizaa matunda katika dk 67 ya mchezo Maliki aliandika bao la kwanza  kwa Azam FC akitumia vema kupotezana kwa mabeki wa Mgambo na kumalizia krosi ya mbali iliyopigwa na beki Erasto Nyoni na kufanya matokeo kuwa Azam FC 1-0 Mgambo.

 

Kasi ya Azam FC haikuishia hapo, walifanya mabadiliko mengine kuimarisha sehemu ya kiungo aliingia Hamis Mcha kuchukua nafasi ya Humprey Mieno, baada ya mabadiliko hayo Azam FC ikacheza katika kiwango kinachotakiwa na kuwapa kibarua mabeki wa Mgambo.

 

Dk ya 86 Azam FC walipata goli la pili kwa mkwaju wa penati iliyopigwa na mshambuliaji Kipre Tchetche, baada ya beki wa Mgambo Ramadhan Kambwili kumwangusha Maliki akiwa katika harakati za kufunga, Maliki kabla kabla ya kuangushwa alitaka kumpita beki wa Mgambo kwa staili ya Zinadine Zidane ndipo peki huyo alipoamua kumkwatua. bao hilo la Kipre lilihitimisha mchezo huo Azam FC ikitoka na ushindi wa 2-0.

 

Ushindi huo unakuwa wa tatu kwa Azam FC tangu kuanza kwa msimu huu wa 2013/2014, iliifunga Rhino Rangers 2-0 na kuifunga Yanga SC 3-1, imetoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Ashanti United na Tanzania Prisons, imetoka suluhu na Coastal Union.

 

Azam FC itashuka tena katika Uwanja wa Azam Complex siku ya Jumamosi kucheza mechi nyingine ya ligi kuu dhidi ya  JKT Ruvu.

 

Azam FC. Mwadini Ally,  Erasto Nyoni, Waziri Salum, Said Morad, Agrey Moris, Michael Bolou, Brian Umony/Farid Mussa Maliki 45’, Salum Abubakar, John Bocco (cpt), Humphrey Mieno/Khamis Mcha na Kipre Tchetche.

 

Mgambo: Tony Kavishe, Daud Salum/Ramadhan Kambwili, Salum Mlima, Bakari Mtama, Bashiru Chanacha, Novat Lufunga, Nassor Gumbo, Mohamed Samata, Mohamed Netto/Malima Busungu, Salum Gilla/Fully Mganga na Peter Mwalyanzi.