Mshambuliaji chipukizi wa Azam FC, Joseph Kimwaga ameifungia timu yake bao la ushindi dhidi ya Yanga katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom ambao Azam FC iliibuka na ushindi wa 3-2 mechi iliyochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Azam FC imeifunga Yanga idadi hiyo ya magoli na kujiongezea pointi tatu muhimu, imefikisha pointi 9 huku Yanga wao wakibaki na pointi zao 6.

 

Hii ni mara ya kwanza kwa kocha wa Azam FC, Stewart Hall kuwajumuisha wachezaji kutoka timu yake ndogo ya Azam Academy, chipukizi ambao wamepeleka furaha katika kikosi hicho chenye maskani yake Azam Complex, Mbagala Chamazi (Mbande).

 

Katika mchezo huo Azam FC ilianza mapema kuandika kalamu ya magoli kupitia kwa nahodha wa kikosi hicho John Bocco aliyefunga goli la kichwa katika dakika ya kwanza ya mchezo baada ya kumalizia mpira uliopigwa na Brian Umony aliyeunganisha krosi ya Humprey Mieno na kuacha mabeki wa Yanga wasijue la kufanya.

 

Zao la bao hilo limetokana na juhudi za mchezaji chipukizi kutoka Azam Academy, Farid Mussa aliyepiga mpira uliotua moja kwa moja kwa Mieno na kumpatia Umony kabla ya Bocco kufunga bao hilo la mapema.

 

Azam FC ilikuwa imara kwa kurejea wachezaji wake Bocco, Umony na Mieno ambao walikuwa majeruhi tangu kuanza kwa msimu huu wa ligi kuu ya 2013/2014.

 

Timu zote zilimaliza kipindi cha kwanza Azam FC ikiongoza 1-0 dhidi ya Yanga ambao walitengeneza na kukosa nafasi nyingi za wazi huku wachezaji Jerryson tegete na Didier Kavumbagu walijaribu na kupiga mashuti yaliookolewa vyema na kipa Aishi Manula wa Azam FC na mengine kutoka nje.

 

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kila timu ilionekana kurekebisha  makosa yake, dk 48 Kavumbagu aliisawazishia Yanga kwa shuti lililowapita mabeki wa Azam FC na kutinga wavuni, goli hilo lilibadilisha matokeo na kuwa 1-1.

 

Kuanzia dakika ya 52 timu zote zilianza kufanya mabadiliko ambayo yalizaa matunda, Azam FC walitoka Brian Umony dk 52 na Jockins Atudo dk 57 nafasi zao zikachukuliwa na Kipre Tchetche na Said Morad, Yanga aliingia Hamis Kiiza dk 60 kuchukua nafasi ya Jerryson Tegete.

 

Yanga dk 65 walipata goli la pili lililofungwa na Kiiza akitumia vyema uzembe wa beki ya Azam FC na kupiga mpira uliotinga moja kwa moja wavuni na kuwapa furaha mashabiki wa Yanga kwa kubadilisha matokeo na kuwa Yanga 2-1 Azam FC.

 

Goli hilo lilidumu kwa dakika nne tu kabla ya mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche kusawazisha katika dk 69 kwa mkwaju wa penati baada ya beki wa Yanga, Kelvin Yondani kuunawa mpira katika eneo la hatari, penati hiyo iliamriwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.

 

Baada ya goli hilo Azam FC walifanya mabadiliko alitoka Farid Musa 71’ nafasi yake ikachukuliwa na Joseph Kimwaga, kuingia kwa mchezaji huyo kuliongeza kasi ya mashambulizi kwa upande wa Azam FC.

 

Kimwaga aliipatia Azam FC goli la tatu na la ushindi akitumia vyema kujisahau kwa mabeki wa yanga na kuachia shuti lilimshinda kipa Ally Mustafa ‘Bartez’ na kuingia wavuni, goli hilo lilimaliza mchezo Azam FC iliyokuwa nyumabani ikipata ushindi wa 3-2 dhidi ya Yanga.

 

Kwa matokeo hayo Azam FC inakuwa imepata ushindi wa pili tangu kuanza kwa ligi kuu 2013/2014 katika mzunguko huu wa kwanza, haijapoteza hata mchezo mmoja, imetoka sare ya 1-1 katika mechi tatu, dhidi ya Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Ashanti United, iliifunga Rhino Rangers 2-0.

 

Kocha Stewart Hall amempongeza Kimwaga kwa kufunga goli la ushindi, ushindi ambao umemuongezea pointi japokuwa timu yake haijacheza katika kiwango kizuri.

 

“Hatujacheza vizuri, Yanga walikuwa wazuri muda wote wamecheza mpira katika kiwango kizuri, lakini mpira ni matokeo tulipata nafasi tukaitumia, kikubwa nampongeza Kimwaga kwa kutupa ushindi” alisema Stewart.

 

Azam FC itaanza maandalizi siku ya Jumatatu kwa ajili ya mechi yake ya  tano ya ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, Septemba 29 mwaka huu.

 

Azam FC: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum, David Mwantika, Jockins Atudo/Said Morad 52’, Himid Mao, Farid Musa/Joseph Kimwaga 71’, John Bocco (cpt), Humprey Mieno na Brian Umony/Kipre Tchetche 57’

 

Yanga SC: Ali Mustafa, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub,Kelvin Yondani, Athuman Idd, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Jerryson Tegete/Hamis Kiiza 60’ na Haruna Niyonzima.