Timu ya Azam FC ipo katika maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kucheza na Kagera Sugar katika mchezo wa ligi kuu utakaochezwa siku ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

 

Azam FC leo asubuhi ilifanya mazoezi yake katika uwanja wa nyasi za kawaida uliopo  Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na www.azamfc.co.tzkocha msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala amesema maandalizi yapo katika hatua za mwisho, wachezaji wapo katika kiwango cha juu kwa ajili ya mchezo huo.

 

Amesema wachezaji wengi wapo vizuri na majeruhi wanaokikabili kikosi hicho wanaendelea vizuri hivyo watanza kuonekana uwanjani hivi karibuni.

 

Aliwataja wachezaji majeruhi kuwa ni John Bocco, Brian Umony, Humphrey Mieno na Aggrey Morris hawa walikuwepo mazoezini isipokuwa Samih Haji Nuhu ambaye hakufika mazoezini kutokana na kusumbuliwa na goti.

 

“Tumefanya maandalizi mazuri yatakayotuwezesha kupata matokeo mazuri katika mechi yetu, kwa sasa tunamalizia sehemu chache ya maandalizi hayo, tumepanga kuanza safari ya kuelekea Kagera siku ya Alhamisi” amesema Kali.

 

Tangu kuanza kwa msimu huu wa 2013/2014, Azam FC imetoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar, ikaifunga 2-0 Rhino Rangers katika mchezo wake wa pili, imefikisha pointi 4, ligi kuu mzunguko wa tatu itaendelea mwisho wa wiki hii, Sept 14, 2013.