AZAM FC leo imepoteza mechi yake ya pili katika ziara yake ya Afrika Kusini baada ya kufungwa mabao 2-1 na Orlando Pirates, kwenye Uwanja wa Randy mjini Johannesburg, nchini hapa.

 

Pichani wachezaji wa akiba wa Azam FC wakiwa wamejifunika mablanketi kutokana na kupigwa baridi kali wakati wa mechi kati yao na Orlando Pirates 

Bao pekee la Azam katika mchezo wa leo lilifungwa na kiungo Jabir Aziz dakika ya 62, wakati wenyeji walipata mabao yao mapema tu dakika ya nne na ya nane.  Awali mchezo huo ulikuwa uchezwe kesho, lakini wenyeji wakaomba uchezwe leo. Na taarifa za awali jana zilikuja mechi itachezwa jioni, lakini asubuhi ya leo Azam FC wakaambiwa wanatakiwa kwenda uwanjani.

Habari na picha kwa hisani ya Blogu ya Binzubeiry iliyopo afrika ya kusini

 

Kocha Stewart Hall aliwaamsha wachezaji wake haraka na kuwapakia kwenye basi kwenda uwanjani.

 

Wazi Azam iliathiriwa na kushitukizwa na kujikuta wanafungwa mabao ya mapema tu, mawili ndani ya dakika ya nanelakini baada ya wachezaji kutulia, Orlando Pirates walikiona cha moto.

 

Kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alitawala sehemu ya kiungo vizuri na John Bocco ‘Adebayor’ aliendelea kupoteza nafasi na hata Gaudence Mwaikimba alipompokea kipindi cha pili, hakuweza kufunga

 

Kipre Tchetche aliiinyanyasa mno ngome ya Pirates, lakini hakuweza kufunga tu. Beki Mkenya Jaockins Atudo ambaye sasa anahimishiwa kulia kutoka katikati, alitia krosi nyingi nzuri.

 

Pamoja na kufungwa mabao mawili ya haraka yaliyotokana na makosa ya Kipre Balou na Ibrahim Mwaipopo, lakini kipa Mwadini Ally alidaka vizuri. Mwadini anaweka rekodi ya kufungwa mabao matano katika mechi mbili alizodaka hapa, kwani ni yeye ndiye aliyesimama langoni timu ikifungwa 3-0 Kazier Chiefs.

 

Kipa wa pili, Aishi Manula alidaka wakati Azam ikishinda 1-0 dhidi ya Mamelodi.   

 

Dakika ya 65 mchezaji mmoja wa Pirates aliunawa mpira kwenye eneo la hatari, lakini refa akawanyima Azam penalti. Kwa ujumla katika mechi zote ambazo Azam imecheza hapa, imekuwa ‘ikiumwa’ na marefa ambao huwa watu wa timu inazocheza nazo.  

 

Baada ya mchezo wa leo, kikosi cha Azam kitacheza mechi yake ya mwisho katika ziara ya hapa Jumatatu dhidi ya Moroka Swallows kabla ya kuondoka Jumanne.

Awali, Azam ilifungwa 3-0 na Kaizer Chiefs Jumatatu kabla a kushinda 1-0 dhidi ya Mamelodi Sundwons juzi

 

Kikosi cha Azam leo kilikuwa; Mwadini Ally, Joackins Atudo/Malika Ndeule dk75, Samih Hajji Nuhu/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk46, Luckson Kakolaki/David Mwantika dk46, Aggrey Morris, Kipre Balou/Himid Mao dk60, Kipre Tchetche/Seif Abdallah dk80, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’/Gaudence Mwaikimba dk46, Ibrahim Mwaipopo/Jabir Aziz dk50 na Waziri Salum.