WASHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Nigeria,  wanaochezea timu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Rafael Chukwu na Muri Ibrahim wanatarajiwa kuwavaa Azam leo katika mechi ya kirafiki ya Kimataifa itakayochezwa kwenye Uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo.

 

Wachezaji wengine wa kulipwa wa Mamelodi  Sundowns ambao watakaonekana katika mechi hiyo ni  mshambuliaji Muivory, Frank Guela  na Mnigeria kiungo Muis Ajao.

 

Azam FC ambayo imeweka kambi ya wiki mbili katikati ya jiji katika Hotel ya Randburg Tower, inajiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, itaanza kucheza na Yanga Agosti 17, mwaka huu, ikiwa ni mechi ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 

Katika mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall anatarajia kuwatumia washambuliaji wake, John Bocco, Khamis Mcha, Abdalla Seifa Karie na Kipre Tchtechte ili waweze kuibuka na ushindi baada ya kupoteza kwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Kaizer Chiefs.

 

Mechi hiyo iliyochezwa Jumatatu wiki hii, kwenye Uwanja wa mazoezi wa Kaizer Chiefs Sport Village uliopo eneo la Naturena, Azam FC ilifungwa mabao 3-0.

 

Azam FC jana iliendelea na mazoezi makali katika viwanja wa Wits kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo, iliyopangwa kuchezwa kuanzia saa tisa jioni kwa saa za hapa.

 

Wachezaji wa timu hiyo, walifanya mazoezi kwa muda wa saa tatu chini ya Kocha wao, Stewart ambaye alionekana kuwa makini katika kuwafua washambuliaji wake.

 

Stewart alitumia mazoezi hayo kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika mechi ya kwanza dhidi ya Kaizer Chiefs baada ya kufungwa na timu hiyo.