AZAM FC leo inatarajiwa kushuka dimbani kwenye Uwanja wa Soccer City, unaojulikana pia kama FNB uliopo Soweto, Johannesburg, Afrika Kusini, kumenyana na wenyeji, Kaizer Chiefs katika mchezo wa kwanza kwenye zaira yake ya kujiandaa na msimu nchini humo.

 

Azam iliyoondoka nchini jana mchana kwa ndege ya Shirika la Afrika Kusini, kwenda Johannesburg, Afrika Kusini kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu mpya, leo itaanza kazi kwenye Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 94,736.

 

Timu hiyo yenye maskani yake, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, iliyoondoka na kikosi chake kizima, kasoro wachezaji wawili tu majeruhi, kiungo Mkenya, Humphrey Mieno na mshambuliaji Mganda, Brian Umony, imefikia katika hoteli ya Randburg Towers.

 

Azam jana ilifanya mazoezi yake ya kwanza kwenye Uwanja wa Wits University asubuhi na jioni na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Muingereza Stewart Hall amefurahishwa na mazingira ya kambi na Uwanja wa mazoezi.

 

“Tumepata mazingira mazuri ya kambi, Uwanja wa mazoezi na mechi nzuri za kujipima nguvu. Vijana watanufaika sana na kambi hii na itakuwa sababu ya kufanya vizuri katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, tukianza na kuchukua Ngao,”alisema.

Baada ya mchezo wa leo, Azam itashuka tena dimbani Agosti 7, kumenyana na Mamelodi Sundowns kabla ya kuivaa Orlando Pirates Agosti 9 na Agosti 12 itamaliza ziara yake kwa kumenyana na Moroka Swallows.

 

Azam inatarajiwa kurejea nchini Agosti 13 tayari kwa mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii kuashiria kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC, Agosti 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 

Safari hii Azam, washindi wa pili mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu wamepania kutwaa Ngao mbele ya Yanga, baada ya mwaka jana kufungwa na Simba SC na kocha Muingereza Stewart Hall anajiandaa kikamilifu kwa ajili hiyo.

 

 

RATIBA YA MECHI ZA AZAM AFRIKA KUSINI:

AGOSTI 5, 2013: 

Azam Vs Kaizer Chiefs 

AGOSTI 7, 2013: 

Azam Vs Mamelodi Sundwons

AGOSTI 9, 2013: 

Azam Vs Orlando Pirates

AGOSTI 12, 2013:

Azam Vs Moroka Swallows 

 

Story kwa hisani ya http://bongostaz.blogspot.com/2013/08/azam-fc-washuka-dimbani-leo-afrika.html