Timu ya Azam FC inatarajiwa kuanza ugenini mechi zake tatu za ligi kuu ya Vodacom (VPL) 2013-2014, itafungua dimba dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Agust 24 mwaka huu.

 

Ratiba hiyo imetolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo Jumatatu, na kuonyesha mzunguko wa kwanza wa ligi unatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 24 Augusti 2013 na kumalizika Novemba 3 mwaka huu.

 

Azam FC watacheza mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) dhidi ya bingwa mtetezi Yanga  Agosti 17 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni wiki moja kabla ya kuanza kwa ligi hiyo inayokutanisha jumla ya timu 14 za ligi kuu ya Tanzania Bara.

 

 

Katika ratiba hiyo, Azam FC itacheza mechi zake tatu ikiwa ugenini, itaanza na Mtibwa Sugar, tarehe 28 August itasafiri hadi mkoani Tabora kucheza na Rhino Rangers ya mkoani humo, timu hiyo imepanda ligi kwa mara ya kwanza msimu huu.

 

Mechi yake ya tatu itakuwa mkoani Kagera kucheza dhidi ya Kagera Sugar tarehe 14 Sept 2013 kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex Chamazi kuwakaribisha Ashanti United hiyo itakuwa Sept 18 mwaka huu.

 

Azam FC itakutana tena na Yanga Sept 22, Uwanja wa Taifa baada ya mechi hiyo Azam FC watasafiri kuelekea Mkoani Mbeya kucheza dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine Sept 29, na Octoba 5 Azam FC itakuwa mgeni wa Coastal Union jijini Tanga.

 

Wawakilishi hao wa Kombe la Shirikisho Afrika, watarejea Azam Complex kucheza dhidi ya Mgambo Shooting ya Tanga Oct 9, na Oct 13 itakuwa mwenyeji wa timu ya JKT Ruvu ya hapahapa jijini Dar es Salaam.

 

Oct 19 Azam FC itacheza mechi yake ya ugenini dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na Oct 27 itakuwa mgeni wa Simba SC kwenye Uwanja wa Taifa.

 

Azam FC itamaliza mzunguko wa kwanza mechi za nyumbani kwenye uwanja wa Azam Complex, Oct 30 itaikaribisha Ruvu Shooting Stars ya kutoka Pwani na Nov 3 itamaliza na Mbeya City kwenye uwanja huo huo.

 

Baada ya mechi hizo Azam FC pamoja na vilabu vyote vya ligi kuu vitakuwa katika mapumziko ya mwezi mmoja kwa maandalizi ya kumalizia mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza Jan 25, 2014 na kumalizika April 27, 2014.