Ushindi wa 3-0 dhidi ya Mgambo Shooting umeipeleka Azam FC CAF Confederations Cup ten  kwa kuwa mshindi wa pili kwenye ligi kuu 2012/2013 na kupata nafasi nyingine ya kuiwakilisha Tanzania kwenye Mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

 

Azam FC imepata ushindi huo wa nyumbani na kufikisha jumla ya pointi 51 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine yoyote iliyo nyuma yake, Azam FC ikitwaa nafasi ya pili, Yanga wiki tatu zilizopita ilitangazwa kuwa bingwa wa ligi hiyo huku Simba wakibaki katika nafasi ya tatu.

 

Mbali na kuwa nafasi ya pili, mshambuliaji wa Azam FC, Tchetche Herman Kipre amezidi kuwaacha wafungaji kwenye ligi kuu na kuwaongoza baada ya kufikisha bao la 17 na kuifanya Azam FC kutoa mfungaji bora kwenye ligi kwa msimu wa tatu mfulilizo, alianza Mrisho Ngassa 2010/12 akafuata John Bocco 2011/2012.

 

Katika mchezo huo Azam FC walianza mapema kulisakama lango la Mgambo ambapo dakika ya 10 na 11 John Bocco aliikosesha magoli timu yake kwa kushindwa kumalizia mipira ya mwisho aliyotengewa na Tchetche.

 

Dk 24 Bocco alirekebisha makosa yake na kuipatia Azam FC bao la kwanza akicheza vizuri crosi ya Humphrey Mieno, aliweza kuwatoka mabeki wa Mgambo na kupiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.

 

Goli hilo la Bocco lilizipeleka timu zote mapumziko Azam FC wakiwa mbele kwa goli 1-0 dhidi ya Mgambo, muda wote wa kipindi cha kwanza Azam FC waliutawala mchezo kwa asilimia kubwa na kutengeneza nafasi nyingi kuliko Mgambo.

 

Kipindi cha pili kilianza timu zote zilianza kwa kasi, Mgambo walianza wakisaka nafasi ya kusawazisha ili kujiweka vizuri lakini wachezaji wake walikosa nafasi nyingi za wazi dk 52 Juma Mwinyimvua alipiga shuti likaokolewa na kipa Mwadini wa Azam FC na dk 56 Issa Kandulu alipiga shuti la mbali likatoka nje.

 

Azam FC walianza taratibu kwa mashambulizi ya mbali ambayo yalizaa matunda katika dakika ya 65 ambapo Kipre aliipatia timu yake bao la pili akiwatoka vyema mabeki wa Mgambo na kupita katikati yao kisha kuachia shuti la mbali lililompita kipa Tonny Kavishe wa Mgambo na kutinga wavuni, matokeo yakawa Azam FC 2-0 Mgambo Shooting.

 

Maafande hao kutoka mkoani Tanga walizidi kupelekeshwa ambapo katika dk 80 beki Jockins Atudo wa Azam FC  aliifungia bao la tatu kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona iliyopigwa kiufundi na Waziri Salum na kupoteza matumaini ya Mgambo Shooting, matokeo yakabadilika na kuwa Azam FC 3-0 Mgambo.

 

Timu zote zilifanya mabadiliko Azam FC walitoka Brian Umony ambaye alifanya kazi nzuri sana ndani ya dk 62 nafasi yake ikachukuliwa na Abdalah Seif Karihe, dk 81 Ibrahim Mwaipopo aliingia kuchukua nafasi ya Michael Bolou na dk 83 Abdi Kassim 'Babi' aliingia kuchukua nafasi ya Humphrey Mieno, Mgambo walitoka Juma Mgunda dk  88 kaingia Omary Matinko na dk 57 alitoka Juma Mwinyimvua nafasi yake ikachukuliwa na Peter Mwalyanzi.

 

Kwa matokeo hayo timu ya Mgambo itakuwa na kibarua kingine cha kusaka pointi moja ili ijinusuru kushuka daraja, huku Azam FC wao wakijiandaa kukamilisha ratiba kwa mchezo wake wa mwisho dhidi ya maafande wengine wa JKT Oljoro utakaochezwa mkoani Arusha.