Baada kurejea nchini, timu ya Azam FC kesho itashuka uwanjani kucheza dhidi ya Mgambo Shooting ikiwa na matumaini ya kupata pointi tatu muhimu zitakazowapa ushindi wa pili kwenye ligi kuu msimu wa 2012/2013.

 

Azam FC inahitaji pointi moja kuweza kujihakikishia kuwa mshindi wa pili kwenye ligi inayoshirikisha timu 14, Azam FC kwa sasa ina pointi 48 inatakiwa kufikisha pointi 49 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote nyingine, wakati Azam FC wakisaka nafasi ya pili, Yanga wiki tatu zilizopita alitangazwa bingwa wa ligi hiyo.

 

Matumaini ya kutwaa pointi zote tatu katika mchezo wao wa kesho dhidi ya Mgambo Shooting ya kutoka Tanga, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, kocha wa Azam FC, Stewart Hall ameiambia www.azamfc.co.tz kuwa wamejiandaa kumaliza wakiwa katika nafasi nzuri hivyo watapata zaidi ya pointi moja.

 

"Huu ni mchezo wetu wa nyumbani, kwetu tunahitaji pointi zaidi ili tumalize tukiwa washindi wa pili tukiwa na pointi nyingi, najua tunahitaji pointi moja ili tuvuke, nimewaambia wachezaji wangu wasiangalie hilo zaidi waangalie kushinda mchezo wa kesho” amesema Stewart.

 

Stewart alisema mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu kwa kuwa kila timu inahitaji pointi, wapinzani wao wanatakiwa kupata pointi moja pia ili waweze kukaa katika nafasi nzuri ya kutoshuka daraja, hivyo mchezo hautakuwa rahisi sana kwa pande zote.

 

"Sidhani kama utakuwa mchezo rahisi, muda huu kila timu inajiangalia na kujiweka sawa kwa nafasi walizonazo, wote tunahitaji ushindi sisi pointi moja na wao pointi moja, ligi inamalizika ikiwa na sura ya aina yake, mechi zote zinaumuhimu” amesisitiza Stewart.

 

Akizungumzia hali za wachezaji wake, kocha Stewart amesema wachezaji Himid Mao, Khamis Mcha, Samih Haji Nuhu wataukosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi, pia wataangalia hali ya Waziri Salum aliyepata majeraha leo asubuhi wakiwa mazoezini.

 

“Wachezaji wote wanahari nzuri, tutapanga kikosi kizuri tu kuweza kupata ushindi, kuwakosa wachezaji hao sio jambo jema lakini tutawatumia mchezo ijao” ameongezea Stewart.

 

Azam FC hadi sasa imejihakikishia nafasi ya pili kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kuwa ina michezo miwili mkononi huku timu inayomfatia ya Simba SC yenyewe ikiwa na mchezo mmoja na inatakiwa ishinde endapo Azam FC itapoteza michezo yote.

 

Endapo Azam FC itashinda itaiwakilisha nchi kwa mara ya pili mfulilizo kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika 2014, kwa mwaka huu ikiwa ni mara yao ya kwanza wameweza kufika hatua ya tatu, wakishinda michezo mitatu, sare mbili na kufugwa mchezo mmoja.

 

Timu hizo zinakutana kucheza mechi zao za mzunguko wa 25, baada ya mechi hiyo kila timu inayoshiriki ligi kuu itakuwa imebakiza mechi moja kuweza kumaliza ligi ambayo itafikia kileleni Mei 18 mwaka huu, huku Azam FC itamaliza ugenini dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.