WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Shirikisho la Afrika (CAF), Azam FC imelazimishwa suluhu na AS FAR Rabat ya Morocco, katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam FC na Rabat zimecheza mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya tatu, kwa matokeo hayo Azam FC bado ina nafasi ya kusonga mbele ingawa ina kibarua kigumu katika mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini Morocco wiki mbili zijazo.

Azam FC walikuwa wa kwanza kilifikia lango la wapinzani wao dakika ya 2, wakati John Boko alipoachia shuti ambalo lilitemwa na mlinda mlango wa Rabat, Ali Grouni.

Rabat katika dakika za mwanzo walionekana kucheza kwa kujihani zaidi wakiwa na lengo la kutafuta sare aina yoyote kutokana na kujazana wengi nyuma kwa mtindo wa kupaki basi.

Mtindo huo wa uchezaji uliwapa tabu Azam FC katika dakika za mwanzo lakini baada ya muda wakapata nafasi ya kutengeneza mashambulizi machache hali iliyopelekea kukosa ushndi katika mchezo huo.

Azam FC ilipunguzwa nguvu dakika ya 6 baada ya mchezaji wake kimataifa kutoka Kenya, Jockins Atudo kugongana na Mustapha Alloui, na kutonesha bega leke linalomsumbua na nafasi yake ikachukuliwa vyema na Luckson Kakolaki.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu katika kipindi cha kwanza ambapo dakikia ya 30 Boko alipoteza nafasi nzuri ya kufunga kwa kupiga mpira uliotoka nje.

Mpaka mwamuzi wa mchezo huo Emile Fred, kutoka Seycheles anapuliza filimbi kuashiria mapumziko hakuna timu ambayo iliyoona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Azam wakionekana kuingia uwanjani kusaka bao la mapema.

Azam ambao walianzisha mashambulizi langoni mwa Rabat, dakika ya 51 Kipre Tcheche alipiga shuti kali lilogonga mwamba baada ya kuunganisha krosi ya Boko na kutoka nje

Dakika moja baadae Khamis Mcha alifanya kazi ya ziada baada ya kuwalamba chenga walinzi wa Rabat na kuachia shuti ambalo lilitoka nje kidogo ya lango.

Rabat kipindi cha pili walionekana kuendelea na mchezo wao wa kulinda huku wakitumia mashambulizi ya kushtukiza.

Kipre Tchetche dk 65 alipata nafasi nyingine akiwa na lango la Rabat alipiga shuti la mbali likagonga mwamba na kurudi uwanjani hatari hiyo ikaokolewa na mabeki wa Rabat.

Dakika ya 88 Waziri Salum alifanya kazi ya ziada baada ya kuwatoka mabeki wa Rabat kuanzia nyumba na kupiga shuti ambalo lilitoa nje mita chache karibu na lango la Rabati nje ya lango.

Katika dakika za nyongeza Kipre tena alipiga shuti ambalo liligonga mwamba na kutoka nje na kuikosesha ushindi Azam FC mabapo mpaka mpira unamalizika matokeo yakawa Azam FC 0-0 AS FAR Rabat.

Azam: Mwadini Ali, John Boko, Himid Mao, Wazir Salum, David Mwantika, Jockins Atudo/Luckson Kakolaki, Balou Kipre, Salum Abubakar, Humphrey Mieno, Kipre Tcheche na Hamis Mcha/Gaudence Mwaikimba.

Rabat: Ali Groun, Mustapha Mrani, Younes Hammal, Younes Bellakhdar, Yassine El Kordy, Abderraddine Said/Mostapha El Yousfi, ,Mohammed El Bakkali, Salaheddine Aqqali/Soufiane Allodi, Mustapha Allaovi na Hicham El Fathi.