Wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, timu ya Azam FC, kesho itashuka uwanjani ikiwa na matumaini ya kusonga mbele kwenye mchezo wao dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco.

Azam FC inawakaribisha Rabat katika mchezo wa kwanza wa hatua ya tatu ya mashindano hayo makubwa Afrika, mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Mchezo huo unaiwekea Azam FC historia kubwa kwa kuwa inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo na kuweza kuvuka vihunzi viwili na kuingia hatua ya tatu ambayo ni hatua ya mafanikio makubwa katika klabu.

Kabla ya kuingia hatua hiyo Azam FC imefanikiwa kuzitoa Al Nasri Juba ya Sudan Kusini kwa jumla ya magoli 8-1 katika hatua ya awali na katika hatua ya pili ikaifungashia virago Barrack YC II ya Liberia kwa magoli 2-1.

Hayo yote ni mafanikio yanayochangiwa na uwezo wa timu kwa ujumla kuanzia uongozi, benchi la ufundi na wachezaji wa klabu hiyo ambayo hadi sasa imejihakikishia nafasi ya kushiriki kombe hilo na mwakani 2014.

Akitoa machache kuhusiana na mechi hiyo kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall ameiambia www.azamfc.co.tzkuwa wamefanya maandalizi mazuri ambayo yataiwezesha timu yake kufanya vizuri hasa katika mchezo huu wa nyumbani.

 

Stewart amesema maandalizi waliyofanya yameangalia zaidi aina ya uchezaji ambayo wapinzani wao Rabat wanautumia.

“Tumewaona kupitia DVD tatu za mechi walizocheza, nilianza mazoezi na wachezaji wangu kuanzia siku ya Jumatatu wameelewa vizuri nina uhakika watafanya vizuri na kuivusha timu kwa kuwa hii itakuwa mechi ngumu kutokana na Rabat kuwa na uzoefu mkubwa kuliko sisi” alisema Stewart.

Stewart amesema katika mchezo huo wachezaji wote wapo vizuri isipokuwa Samih Haji Nuhu ambaye ni majeruhi pamoja na Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Said Morad na Deogratius Mushi ambao kwa pamoja wataikosa mechi hiyo kutokana na majina yao kutopelekwa kwenye usajili wa CAF.

Azam FC baada ya mechi ya kesho wiki mbili zijazo itasafiri kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya mchezo wa marudiano ambapo mshindi atavuka na kuingia hatua ya 16 bora.

Wachezaji wa Azam FC watakaiwakilisha klabu na nchi kwa ujumla katika mchezo huo ni Mwadini Ally, Aishi Salum, Himid Mao, Waziri Salum, Luckson Kakolaki, David Mwantika, Jockins Atudo, Jabir  Aziz, Michael Bolou, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Tchetche Kipre, Abdi Kassim ‘Babi’, Ibrahim Mwaipopo, Khamis Mcha, Humphrey Mieno, Brian Umony, Gaudence Mwaikimba, Seif Abdalah ‘Karihe’, Omray Mtaki, Malika Ndeule, John Bocco na Uhuru Seleman.