Timu za Azam FC na Simba zimeshindwa kutambiana baada ya kumaliza mchezo wa ligi kuu ya Vodacom (VPL) kwa sare ya 2-2 kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

 

Matokeo ya mchezo huo yameipatia kila timu pointi moja moja, Azam FC ikifikisha pointi 47 huku Simba wao wakifikisha pointi 38 kwenye msimamo wa ligi kuu unaoongozwa na Yanga yenye pointi 52.

 

Mchezo huo uliovuta hisia za mashabiki wengi kwa kuwa matokeo ya leo yalikuwa yanabadilisha muonekano mzima wa ligi kuu kwa Azam FC wangeshinda wangejiweka pazuri kusaka ubingwa na nafasi ya pili na kama wangefungwa wangepoteza matumaini ya ubingwa.

 

Katika mchezo huo Azam FC walibadilisha mfumo wa uchezaji na kuanza na mabeki watano hali ambayo sio ya kawaida, iliwafanya wachezaji wachanganyane na kuruhusu mashambulizi mengi.

 

Simba walikuwa wa kwanza kupata magoli yote mawili, goli la kwanza lilipatikana dakika ya 11 ya mchezo huo kupitia kwa mshambuliaji Ramadhan Singano aliyecheza vizuri krosi ya Mrisho Ngasa  na kuunga goli hilo matokeo yakawa 1-0.

 

Singano aliipatia Simba bao la pili katika dakika ya 18 akimalizia tena mpira uliopigwa na Ngasa aliyemtoka beki wa Azam FC Luckson Kakolaki, Simba ikaongoza 2-0.

 

Azam FC walifanya mabadiliko ya kwanza na ya ufundi dakika ya 21 ya mchezo huo alitoka Kakolaki nafasi yake ikachukuliwa na Khamis Mcha aliyebadili mchezo huo kwa kiasi kikubwa.

 

Mabadiliko hayo yaliiamsha Azam FC na kufanya mashambulizi mengi, dakika ya 29 Kipre Tchetche akaipatia Azam FC bao la kwanza kwa mkwaju wa penati iliyoamriwa na mwamuzi Oden Mbaga baada ya beki Miraji Mdigo kumtendea madhambi Mcha kwenye eneo la hatari, matokeo yakabadilika na kuwa Azam FC 1-2 Simba.

 

Hilo ni bao la 16 kwa mshambuliaji Kipre Tchetche ambaye amezidi kuwaacha wafungaji wengine kwenye ligi kuu na kujihakikishia nafasi ya kutwaa kiatu cha dhahabu.

 

Dakika ya 33 mwamuzi wa kati Mbaga alimtoa kwa kadi nyekundu kocha wa Azam FC, Stewart Hall kwa kukiuka sheria za kukaa benchi, tangu mda huo timu ikawa chini ya makocha wasaidizi Kali Ongala na Ibrahim Shikanda.

 

Kipindi cha kwanza kilimalizika Simba wakiongoza 2-1 dhidi ya Azam FC, baada ya mapumziko kila timu ilirejea uwanjani ikiwa na kasi zaidi ya ile ya kipindi cha kwanza.

 

Azam FC walibadili aina ya uchezaji na kucheza katika kiwango kizuri tofauti na kipindi cha kwanza, hali iliyowafanya kutengeneza nafasi nyingi zaidi.

 

Dakika ya 71 Humphrey Mieno akaipatia Azam FC bao la kusawazisha akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Mcha kufuatia mchezaji wa Simba Mussa Mude kumwangusha Kipre nje ya eneo na la hatari na kubadilisha matokeo kuwa 2-2.

 

Azam FC walifanya mabadiliko dk 80 alitoka John Bocco nafasi yake ikachukuliwa na Abdi Kassim 'Babi' na dakika ya 85 aliingia Jabir Aziz kuchukua nafasi ya Humprey Mieno mabadiliko hayo yaliongeza kasi kwa Azam FC.

 

Simba nao waliwatoa William Lucian, Haruna Chanongo na Mrisho Ngassa nafasi zao zikachukuliwa na Mwinyi Kazimoto, Edward Christopher na Felix Sunzu mabadiliko hayo hayakuweza kubadilisha matokeo na mpira ukamalizika Azam FC 2-2 Simba SC.

 

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo kocha wa Azam FC, Stewart Hall aliiambia www.azamfc.co.tz kuwa anabeba lawama zote za kupata sare hiyo kwa kuwa alibadilisha kikosi ambacho kilishindwa kufanya kazi vizuri.

 

“Nabeba jukumu la kutoka sare, nilibadilisha mfumo ambao mazoezini ulifanya vizuri lakini hapa umefanya vibaya, nilibadilsha timu tukafanikiwa kupata sare, sasa tuna uhakika wa nafasi ya pili tunasubiri nafasi ya kwanza” alisema kocha Stewart Hall.

 

Azam FC itaingia kwenye maandalizi kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho  Afrika dhidi ya FAR Rabat ya Morocco utakaochezwa kati ya tarehe 19,20 na 21 April mwaka huu.

 

Azam FC Mwadini Ally, Himid Mao Mkami, Waziri Salum, Jockins Atudo, Luckson Kakolaki/Khamis Mcha Viali 21', David Mwantika, Michael Bolou, Salum Abubakar 'Sure Boy', Humphrey Mieno/ Jabir Aziz 85', Tchetche Kipre na John Bocco (cpt) /Abdi Kassim 'Babi' 80'.

 

Simba SC Abel Dhaira, Nassor Masoud, Miraji Mdigo, Mussa Mude, Shomari Kapombe, Abdalah Seseme, William Lucian/Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo, Mrisho Ngassa/Felix Sunzu, Amri Kiemba na Ramadhan Singano.