Masaa machache kabla ya kushuka uwanjani kucheza dhidi ya Simba SC, kocha wa Azam FC Stewart Hall amesema kikosi chake kipo kamili kuhakikisha hakipoteza mchezo huo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Azam FC na Simba zitakutana katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara (VPL) kila moja ikisaka pointi za kujiweka vizuri kwenye ligi kuu ikiwa imesalia mizunguko mitatu kumalizika.

 

Endapo Azam FC itashinda mchezo wa leo itafikisha pointi 49 ambazo haziwezi kufikiwa na Simba hivyo Kagera Sugar itabaki kama timu pekee inayoweza kufikisha pointi 49. Azam FC inaizidi Kagera Sugar magoli 14 idadi ambayo ni ngumu kwa kagera kuigeuza kwa mechi nne zilizosalia. kwa maana hiyo Azam FC itakuwa imejihakikishia nafasi ya pili na kutimiza malengo yake iliyojiwekea msimu huu.

 

Akizungumza na www.azamfc.co.tzkocha Stewart amesema ameandaa kikosi maalum cha kuikabili Simba kwa kuwa anajua watachezesha wachezaji wao muhimu katika mchezo huo utakaobadilisha muonekano wa ligi kuu.

 

“Ni mchezo mgumu wote tunatafuta pointi, naimani wachezaji wangu watafanya vizuri kutokana na maandalizi tuliyopata wenzetu wanaweza kutumia wachezaji wakubwa sisi tumejiandaa kwa kila timu wakiweka vijana ama wakubwa tutapambana nao” amesema Stewart.

 

Ameongeza kuwa mchezo huo ni muhimu kushinda na wana kila sababu ya kushinda ili kupata pointi tatu zitakazowaweka karibu kusaka ubingwa wa ligi kuu.

 

“Simba wapo nyuma yetu kwa pointi 11, tunaangalia kupata pointi tatu zitakazotusogeza karibu na kupunguza nafasi kati yetu ya Yanga waliombele kwa pointi 6” amesema Stewart.

 

Akizungumzia kikosi kitakachoshuka uwanjani kesho Stewart amesema wote watakao kuwa fit watacheza akiwepo golikipa Mwadini Ally.