Timu ya Azam FC imeendeleza ushindi kwenye ligi kuu ya Vodacom baada ya kuichapa African Lyon 3-1 katika mchezo uliochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Pichani Juu wachezaji wa Azam FC Himid Mao na Jabir Aziz wakimpongeza mwenzao Kipre Tchetche baada ya kufunga goli la tatu, Picha kwa hisani ya Blogu ya Binzubeiry

 

Kwa ushindi huo, Azam FC imefikisha jumla ya pointi 46 na kujiimarisha katika nafasi ya pili juu kwenye msimamo wa ligi kuu ikizidiwa na Yanga kwa pointi tatu.

 

Katika mchezo huo Azam FC walianza mapema kusaka goli na kufanikiwa kupata bao la kwanza katika dakika ya 8 ya mchezo huo likifungwa na Khamis Mcha Viali aliyemalizia kazi nzuri ya Kipre Tchetche.

 

Azam FC wakiongoza 1-0 walizidisha mashambulizi huku kipa wao katika mchezo huo akiwa Aishi Salum kutoka kikosi cha Azam Academy aliyemudu mchezo huo.

Tchetche akitumia vema kosa la mabeki wa Lyon kujisahau na kudhani ameotea, alitumia nafasi hiyo kumpiga chenga kipa wa Lyon Noel Lucas na kufunga goli la pili kwa Azam FC dakika ya 28 matokeo yakawa Azam FC 2-0 Lyon.

Adam Kingwande aliipatia Lyon bao dk 34 kwa shuti la mbali baada ya kufanikiwa kupenya kwenye ngome ya Azam FC na kupiga mpira uliotinga moja kwa moja wavuni na kupeleka timu mapumziko Azam FC wakiwa 2-1 dhidi ya Lyon.

Azam FC ikiwa chini ya nahodha wake Salum Abubakar ‘Sure Boy’ waliutawala mchezo kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi nyingi ambazo hawakufanikiwa kupata goli.

 

Jabir Aziz alijaribu kupiga shuti dk 21 na Waziri Salum lakini hawakuweza kuipatia goli timu yao baada ya mashuti yote kutoka nje.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, Lyon wakisaka nafasi ya kusawazisha na kupata ushindi ili wajinasue kushuka daraja, walijikuta wakipoteza nafasi nyingi za wazi.

Azam FC walifanya mabadiliko dk 59 alitoka Ibrahim Mwaipopo nafasi yake ikachukuliwa na Humphrey Mieno, dk 55 Khamis Mcha alirejea benchi akaingia Brian Umony.

Mabadiliko hayo yalikuwa na manufaa makubwa kwa Azam FC ambao dk 61 Tchetche aliongeza bao la tatu kwa Azam FC akicheza vizuri pasi ndizi au bakuli fupi iliyopigwa na Mieno na kubadili ubao wa matokeo kusomeka 3-1 hadi mwisho wa mchezo huo.

Tchetche amezidi kupaa na kuwaacha washambuliaji wa ligi kuu ya Vodacom (VPL) kwa kufikisha jumla ya magoli 15.

Mchezo huo ulimalizika Azam FC wakipata ushindi mwingine  na kujiongezea pointi tatu ikipata uhakika wa kubaki katika nafasi mbili za juu.

Azam FC siku ya Jumapili itashuka uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza mchezo mwingine wa ligi kuu dhidi ya Simba SC.

Azam FC, Aishi Salum, Himid Mao, Waziri Salum, Luckson Kakolaki, Jockins Atudo, Jabir Aziz, Kipre Tchetche, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Abdi Kassim ‘Babi’/Seif Abdalah ‘Karihe’ 74’, Ibrahim Mwaipopo/Humphrey Mieno na Khamis Mcha Viali/Brian Umony.