Azam FC ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, huenda wakabaki kuwa wawakilishi pekee wa ukanda wa Afrika mashariki baada ya timu nyingi toka ukanda huu zikiwa zimeaga mashindano hayo na zile zilizosalia zinasubiri maajabu katika mechi zinazochezwa leo.

Timu ya Azam FC, jana ilifanikiwa kutinga raundi ya mwisho ya 16 bora baada ya kuing’oa Barrack Young Controllers II ya Liberia katika mbio za Kombe la Shirikisho.

Azam ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa baada ya Simba na Jamhuri kuaga hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wamevuka kikwazo kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1. Kufuatia kuichapa BYC ll 2-1 kule Liberia na jana kwenda sare ya 0-0

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC inayonolewa na Kocha Stewart John Hall kuzidi kupeta licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa tangu kuasisiwa kwao Juni 24, 2007.

Ushindi huo unaifanya Azam kukutana na timu kongwe na Mabingwa wa Afrika  mbara mbili mwaka 1985 na 2005 FAR Rabat inayomilikiwa na jeshi la Morocco ambapo mechi ya kwanza itachezwa wiki mbili zijazo kati ya Aprili 19 na 21 kabla ya kurudiana kati ya Mei 3 hadi 5.

Kwa mujibu wa muundo wa michuano hiyo, mshindi wa jumla kati ya Azam na FAR Rabat, ataingia kwenye hatua ya mtoano itakayojumuisha timu 16; zikiwemo nane zilizoaga raundi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Tofauti na Azam inayocheza mara ya kwanza michuano ya kimataifa, FAR Rabat iliyoanzishwa 1958, ni timu kongwe iliyowahi kutwaa ubingwa wa michuano hii mwaka 2005 na Ligi ya Mabingwa (wakati huo Klabu Bingwa Afrika) mwaka 1985.

Mwaka 2006, FAR Rabat inayoshiriki kwa mara ya tano Kombe la Shirikisho, ilifika fainali ya michuano hii kabla ya kung’oka raundi ya kwanza mwaka 2010.

Zaidi ya hapo, mwaka 1986 ilifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na miaka miwili baadaye kuishia hatua ya nusu fainali.

FAR Rabat inamiliki uwanja wa Moulay Abdellah wenye uwezo wa kubeba watu 60,000.

Katika mechi ya jana, licha ya timu hizo kushambuliana kwa nguvu hivyo kuwepo kwa kosa kosa nyingi hasa katika lango la Barrack, dakika ya 39, Jockins Atudo alikosa bao baada ya mpira wake wa kisigino kugonga mwamba na kurejea uwanjani.

Mpira huo ulimkuta Kipre TcheTche ambaye alifumua shuti ambalo halikuweza kuzaa bao.

Dakika ya 45, Cammue Tummomie wa Barrack alilimwa kadi ya njano kwa mchezo mbaya.

Barrack walifanya kazi ya ziada kuokoa shuti ya Hamis Mcha iliyotokana na mpira wa adhabu ndogo dakika ya 52, lakini mpigaji akipatwa na kigugumizi cha mguu kabla ya Bocco kushindwa kuutumia vizuri mpira uliokuwa ukirudi.

Dakika ya 60, Tchetche alipiga shuti ambalo lilidakwa vibaya na kipa wa Barrack, Winston, na dakika sita baadae akakosa bao la wazi akiwa na kipa.

Azam: Mwadini Ally, Himid Mao, Wazir Salum, Jockins Atudo, David Mwantika, Kipre TcheTche, Salum Aboubakar, John Bocco, Humphrey Mieno na Brian Umony.

Barrack: Wiston Sayouh, Karleo Anderson, Joseph Broh, Cammue Tummomie, Prince Jetoh, Junior Barshall, Benjamin Gbamy, Abraham Andrews, Randy Dukuly, Maric Paye na Ezekiel Doe.

Habari hii ni kwa msaada wa gazeti la Tanzania Daima